• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wahasiriwa wa dhuluma za polisi Corona ikitesa wataka fidia

Wahasiriwa wa dhuluma za polisi Corona ikitesa wataka fidia

NA RICHARD MUNGUTI

JAMAA wa wahanga wa ukatili wa maafisa wa polisi waliouawa katika mazingira ya kutatanisha 2020 wakati wa kutekeleza sheria za kafyu wakati wa janga la Corona wameishtaki Serikali wakiomba walipwe fidia ya zaidi ya Sh100 milioni.

Miongoni mwa wahasiriwa hao ni Vitalis Owino ambaye polisi walipiga risasi akikojoa nje ya nyumba yake katika mtaa wa mabanda wa Mathare, Nairobi.

Mbali na Vitalis, aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la nane Yassin Hussein Moyo alipigwa risasi akiwa amesimama katika dari ya nyumba yao mtaani Huruma akiwa na mama yake mwendo wa saa moja jioni.

Naye Elvis Emmanuel Otieno alikumbana na polisi waliokuwa wakishika doria Mathare na bila kumwuliza swali walimmiminia risasi na kumwangamiza.

Pamoja na hao Joseph Siminyu naye alishambuliwa na kuachwa amelemaa na polisi waliomtandikia barabarani wakidai anakaidi sheria za kafyu wakati wa gonjwa hatari la Corona almaarufu Covid-19.

Katika kesi iliyowasilishwa na Kituo cha Sheria kupitia wakili mkongwe na mwenye tajriba ya juu katika masuala ya sheria Dkt John Khaminwa na wakili John Mwariri walalamishi hao wanaomba mahakama kuu iamuru serikali iwafidie zaidi ya Sh100 milioni.

“Wahasiriwa hawa wa ukatili wa polisi waliathirika pakubwa tangu wapendwa wao wauawe ama kujeruhiwa na polisi bila sababu. Naomba hii mahakama kuu ipitishe uamuzi kwamba polisi walikatiza maisha ya wahasiriwa pasipo na uchokozi wowote,” Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Enock Chacha Mwita wakati wa kuanza kusikizwa kwa kesi hiyo ya wahanga wa ukatili wa polisi.

Dkt Khaminwa aliwasilisha mashahidi ambao walitoa ushuhuda kuhusu shida walizopata tangu wapendwa wao wauawe au kuumizwa na polisi.

Bw Hussein Moyo Monte, babaye marehemu Yassin Hussein Moyo, mwanafunzi wa darasa la nane aliyepigwa risasi na polisi akiwa amesimama katika dari ya oghorofa ya pili ya makazi yao Huruma Nairobi.

Bw Monte alimweleza Jaji Mwita kwamba polisi walikatiza maisha ya mwanaye.

“Nilikuwa na matumaini makubwa na mwanangu marehemu. Alikuwa kioo cha familia yangu kutokana na bidii yake kwenye masomo. Maisha yake yalikatizwa bure kabisa na afisa wa polisi waliyemlenga na kumfyatulia risasi pasi na uchokozi wowote,” Bw Monte alieleza Jaji Mwita akitoa ushahidi Jumatatu, Aprili 8, 2024.

Baba huyo alisema maisha katika familia yake yaligeuka kuwa ya huzuni na kupotelewa na ufahamu.

Alisema kwa muda mrefu alipatwa na shinikizo la damu na mkewe aliathiriwa mno na kuuawa kwa mwanawe.

“Mke wangu na Yassin walikuwa wamesimama mwendo wa saa moja jioni wakati afisa mmoja wa polisi alipowawelekea bunduki na kufyatua risasi iliyomgonga mwanangu na kumuua papo hapo,” Bw Monte alimweleza Jaji Mwita.

Mzazi huyo alisema mwanawe alikuwa akisoma katika shule ya msingi ya Dururumo alipopatwa na janga hilo.

“Mwanangu alikuwa afanye mtihani wa Kitaifa Darasa la Nane, KCPE 2020 lakini hakuishi kutekeleza ndoto yake,” Bw Monte alimweleza Jaji Mwita.

Naye Bi Evelyn Akinyi alitoa ushahidi huku akilengwalengwa na machozi jinsi mumewe Vitalis Owino aliuawa na polisi akijisaidia haja ndogo nje ya nyumba yao katika mtaa wa mabanda wa Mathare.

“Tangu polisi wamuue mume wangu tumeteseka sana mimi na watoto tuliojailiwa kuwapata,” Akinyi aliambia Jaji huku akishindwa kuutoa ushahidi kwa sababu ya majonzi.

Jaji Mwita alielezwa na mjane huyo kwamba mumewe alikuwa akichumia familia yake na tangu auawe “wanaishi maisha ya uchochole”.

Simiyu anayetembea kwa msaada wa fimbo alieleza mahakama alichapwa na kuumizwa na polisi waliokutana naye akiharakisha kurejea nyumbani asikamatwe kwa kukaidi sheria za kafyu.

Bi Judy Simiyu alieleza mahakama nduguye Elvis Emmanuel aliuawa na polisi waliompiga risasi bila sababu.

Mahakama ilielezwa polisi walikiuka sheria walipoua wahasiriwa hao.

Jaji Mwita aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge waonywa dhidi ya kupitisha mswada unaoharamisha...

Jinsi wanafunzi wa chuo walivyong’ang’ania Githeri...

T L