Habari za Kitaifa

Magavana wakataa kuajiri wahudumu wa afya wa UHC kama alivyoagiza Duale

Na LEON LIDIGU August 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KAUNTI zote 47 zimekataa kwa kauli moja agizo la Waziri wa Afya Aden Duale la kuwaajiri kazi ya kudumu na pensheni wahudumu wa afya walioajiriwa chini ya mpango wa afya kwa wote UHC kuanzia Septemba 1, 2025.

Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana (CoG), Gavana Muthomi Njuki, alikataa agizo hilo akitaja sababu kuu nne kama vile ukosefu wa mashauriano, kutokuwepo orodha halisi ya wahudumu waliothibitishwa, kutotolewa kwa Sh7.7 bilioni zilizokubaliwa, na malimbikizi ya malipo ya marupurupu ya wahudumu hao wa afya.

“Uhusiano kati ya Wizara ya Afya na serikali za kaunti unapaswa kuwa wa ushirikiano, si amri,” alisema Gavana Njuki kwa wanahabari Nairobi, akimkosoa Waziri Duale kwa kutangaza uamuzi bila kushauriana na CoG.

Mgogoro huu unahusu hatma ya wahudumu wa afya 8,571 walioajiriwa na Wizara ya Afya mwaka wa 2020 wakati wa janga la Covid-19 na kutumwa kwa kaunti zote.Uchunguzi wa pamoja kati ya Wizara ya Afya na Baraza la Magavana ulifichua udanganyifu mkubwa kwenye mpango wa UHC.

Katika zoezi hilo, ilibainika kwamba baadhi ya watu waliodaiwa kuwa wahudumu wa afya ni watu wasio na mafunzo ya udaktari kama mafundi bomba, wasusi, seremala, na walimu wa shule za chekechea.

“Baraza la Magavana linatambua ushirikiano unaoendelea baina ya serikali kuu na za kaunti kuhusu usimamizi wa wafanyakazi wa UHC, lakini linapinga msimamo wa Wizara ya Afya uliotolewa kupitia taarifa kwa vyombo vya habari,” alisema Gavana Njuki.

Zoezi la uthibitishaji, lililokamilika wiki iliyopita, lililenga kuwaondoa angalau “wafanyakazi hewa” 3,000, na liliwaacha maafisa wengi wakiwa na mshtuko kuhusu kiwango cha ulaghai uliokuwepo.

Kwa mujibu wa Bw Njuki, Kenya imepoteza angalau Sh9 bilioni katika kipindi cha miaka mitano, kuwalipa mishahara watu wasiofanya kazi halali. Kwa wastani wa mshahara wa Sh50,000 kwa mwezi kwa kila mhudumu, wafanyakazi hewa 3,000 walisababisha hasara ya Sh150 milioni kwa mwezi, sawa na Sh9 bilioni kwa miaka mitano.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika kaunti 18 zikiwemo Trans Nzoia, Bungoma, Narok, Bomet, Baringo, Elgeyo Marakwet, Kisii, Migori, Tana River, Garissa, Nairobi, Makueni, Samburu, Laikipia, Taita Taveta, Kwale, Murang’a, na Kirinyaga ulionyesha kuwa ni kaunti ya Baringo pekee iliyoweza kuthibitisha 186 kati ya wahudumu 187 kuwa halali, huku mmoja akishindwa kufika kwenye zoezi la uthibitishaji.

Akizungumza awali mwezi huu mjini Eldoret, Waziri Duale alikiri kuwepo kwa wafanyakazi hewa na akaahidi kuchukua hatua kali.Waziri huyo wa Afya alionya kuwa wale waliolipwa bila sifa za kitaaluma watalazimika kurejesha mishahara yao ya miaka mitano, na akaahidi kuwasilisha majina yao kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).“Kuna maelfu ambao ni wafanyakazi hewa,” Bw Duale aliwaambia wahudumu hao.

“Kwa sasa, kwa mujibu wa takwimu nilizonazo, nitawasilisha majina ya wengi wenu kwa EACC kwa sababu tofauti ya idadi ya waliopo kazini na waliolipwa ni ya kushangaza.

”Baraza la Magavana limetaja masharti maalum yanayopaswa kutimizwa kabla ya kuanza kwa mchakato wowote wa kuwaajiri wahudumu wa UHC. Gavana Njuki alisisitiza kuwa Wizara ya Afya haijatoa orodha ya wahudumu waliothibitishwa baada ya zoezi la uhakiki.

“Kuhusu uhamisho wa wafanyakazi wa UHC, ilikubaliwa kuwa Wizara ya Afya itatenga rasilmali za kutosha kulingana na viwango vya mishahara vilivyoidhinishwa na Tume ya Mishahara kabla ya kuhamisha majukumu kwa kaunti,” alisema.

Kaunti pia zinataka malipo yote ya marupurupu yaliyocheleweshwa yalipwe kikamilifu kwanza.“Wahudumu wa UHC walioko kwenye mikataba wanastahili kulipwa marupurupu yao. Wizara ya Afya inapaswa kulipa hayo kabla ya kuhamisha wafanyakazi kwa kaunti,” Bw Njuki alieleza.

Gavana Njuki alimkumbusha Waziri Duale kuwa Katiba ya Kenya inataka ushirikiano na mashauriano kati ya serikali kuu na za kaunti, si maagizo ya upande mmoja.

“Baraza la Magavana linapendekeza kuwa serikali kuu, kupitia Wizara ya Afya, itenge na kusambaza rasilmali zinazohitajika kwa serikali za kaunti, ili kuwezesha kuwaajiri wahudumu wa UHC kulingana na sera zao za rasilimali watu. Kinyume chake, hatua hiyo haitatekelezeka,” alionya.