Habari za Kitaifa

Wahuni wachafua urejeo wa Gachagua; ashindwa hata kuzungumza

Na NDUBI MOTURI August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, Bw Rigathi Gachagua, alirejea nchini jana na kupokelewa na wafuasi wake waliokuwa wamepiga kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) usiku kucha.

Licha ya furaha ya kumpokea kiongozi wao, msafara wao ulishambuliwa na wahuni na akakosa kuelekea uwanja wa Kamukunji ambako alikuwa amepangiwa kuhudhuria mkutano wa kisiasa.

Gachagua alijaribu kujificha miongoni mwa wasafiri wengine, lakini wafuasi wake walikuwa macho.

Huku nyimbo za ‘wantam’ zikisikika kila kona, hali ya taharuki ilianza kutanda baada ya taarifa kuenea kwamba Gachagua hangepitia lango kuu la kuwasili kama ilivyotarajiwa.

Wafuasi wake walianza kuelekea lango moja hadi jingine, wakijaribu kumtambua kiongozi wao.

Ndani ya dakika chache, sintofahamu ilitanda uwanjani, na abiria waliokuwa hawana habari kilichokuwa kikiendelea walijikuta katikati ya fujo.

Macho yote yakageukia upande wa eneo linalotumiwa na watu mashuhuri, ambapo ilihofiwa kuwa polisi walikuwa wamepanga kumkamata naibu huyo wa rais wa zamani.

Wakati huo huo, Naibu Kiongozi wa Chama cha Democracy for Citizens (DCP), Cleophas Malala, alijaribu kuingia katika eneo la watu mashuhuri lakini akazuiwa.

Hilo liliibua mzozo mkubwa, huku Malala akiishutumu serikali kwa kupanga njama ya kumkamata Gachagua.

“Wanataka kumkamata kiongozi wetu. Hatutaruhusu jambo hilo litokee. Hatutaondoka hapa bila yeye,” aliwaambia wafuasi waliokuwa wakijaribu kulazimisha kuingia ndani.

Hatimaye, Gachagua alitokea akiwa amezingirwa na walinzi wake. Wafuasi wake walilipuka kwa shangwe, wakiimba nyimbo za kumsifu na kupiga video kwa simu zao.

Gachagua hakusema lolote kwa wakati huo, bali alinyanyua mkono kwa ishara ya salamu kabla ya kuingia kwenye gari lake.

Msafara wa magari ya kifahari ulianza kutoka uwanjani, huku ukifuatwa na mamia ya wafuasi waliojaa furaha.

Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla walipofika eneo la Cabanas kwenye Barabara ya Mombasa. Wahuni waliokuwa wamejificha walijitokeza na kuanza kushambulia msafara huo kwa mawe.

Waliweka mawe barabarani na kuzuia magari kupita. Vioo vya magari vilivunjwa huku walinzi wa Gachagua wakijaribu kuzuia mashambulizi kwa marungu.

Kwa dakika chache, hali ya hatari ilitanda. Baada ya hali kutulia na msafara kupita, viongozi waliokuwa kwenye magari hayo walitoa matamshi makali kulaumu serikali.

Seneta wa Nyandarua, John Methu, alimlaumu Rais William Ruto kwa kupanga mashambulizi hayo.

“Usijifiche nyuma ya wahuni na maafisa wa polisi. Kwa nini uagize mashambulizi dhidi ya raia wenye amani?” aliuliza.

Cleophas Malala naye alidai polisi zaidi ya 180 walitumwa JKIA kwa nia ya kumkamata Gachagua.

“Tulikuja kumpokea kiongozi wetu, lakini serikali ikatumia hila na nguvu kujaribu kutuzuia. Tunataka haki na kuheshimiwa kwa Katiba,” alisema.

Mbunge wa Manyatta, John Mukunji, alishutumu vikali serikali ya Rais Ruto, akisema imepoteza uhalali na maadili.

“Rais Ruto hana haki ya kutufundisha kuhusu maadili, ufisadi wala ukabila. Anawezaje kutumia polisi na vitoa machozi dhidi ya watu waliokuja tu kumpokea kiongozi wao?” alisema.

Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu, alidai kuwa helikopta moja ya serikali ilitumika kuratibu mashambulizi ya wahuni waliovamia msafara wa Gachagua.

“Na ijulikane wazi, Rigathi Gachagua ni kiongozi wetu halali. Tunampenda, na hatutaacha kusema ukweli,” alisisitiza.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya, alitaja tukio hilo kama uvunjaji wa haki za msingi.

“Hii ni siku ya huzuni. Serikali inawageukia wananchi wake kana kwamba ni wageni. Gavana Sakaja, tunajua ulihusika,” alidai kwa hasira.

Licha ya hali hiyo ya vurugu, Gachagua hakuzungumza na umma. Aliendelea na safari yake kimya kimya, huku washirika wake wakitoa matamshi makali dhidi ya serikali.

Ukimya wake ulimaanisha mengi kwa wafuasi wake waliotafsiri kuwa ni ishara ya uthabiti na kujizuia.

Msafara wake uliingia barabara ya Southern Bypass na kuelekea Karen badala ya Kamukunji na kati kati ya jiji ilivyotarajiwa.

Mnamo Jumatano, polisi walitangaza kuwa iwapo Gachagua atahusishwa na makosa yoyote ataandikisha taarifa, kauli ambayo iliongeza hofu kwamba angekamatwa hasa baada ya kauli za Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Naibu Rais Kithure Kindiki ambao walidai ni hatari kwa usalama wa nchi.