Habari za Kitaifa

Waislamu wahimizwa kuhifadhi Qur’an kupalilia tabia njema

March 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ABDULRAHMAN SHERIFF Na KARIM RAJAN

WAUMINI wa Kiislamu nchini wametakiwa kuzingatia mafundisho ya dini kwani yanachangia pakubwa katika kujenga mtu kimaadili. 

Akizungumza akiwa mgeni wa heshima katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an katika uwanja wa Makadara jijini Mombasa, Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim Hussein alisema mafunzo ya dini yanayotolewa kwenye misikiti na madrassa, yamesaidia pakubwa kurekebisha tabia za vijana.

“Mafunzo ya dini ya Kiislamu yamewasaidia vijana kwa kiasi kikubwa kujiepusha na utumiaji wa dawa za kulevya na magenge ya uhalifu ambayo yanachangia ukosefu wa usalama,” akasema Sheikh Hussein.

Aidha Kadhi Mkuu aliwahimiza waumini kuutumia vyema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kujishughulisha na ibada, kusoma Qur’an kwa wingi na kuepukana na vitendo ambavyo vitawachumia madhambi badala ya fadhila.

Sheikh Hussein pia aliwataka Waislamu kuwekeza zaidi katika kuhifadhi na kusoma Qur’an huku akibainisha mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu yanasaidia waumini wapate kutekeleza maadili mema yanayotakikana kufuatwa katika shughuli za maisha ya kila siku.

Washindi katika kategoria mbalimbali za mashindano ya kuhifadhi Qur’an wakiwa na zawadi zao katika uwanja wa Makadara, Kaunti ya Mombasa. PICHA | ABDULRAHMAN SHERIFF

Mashindano hayo ya siku tatu yalijumuisha wanafunzi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania na visiwa vya Zanzibar, Uganda, Somalia, Burundi, Congo, na Rwanda. Wanafunzi waliwekwa katika vitengo vinne vya kuhifadhi Juzuu tano, 10, 20, na 30.

Katika mashindano hayo ya makala ya 20 yaliyotayarishwa na Muslim Mercy Youth (MMY), Yunus Masoud wa Markaz Aldaawa kutoka Ukunda, aliibuka mshindi wa hapa nchini Kenya wa kuhifadhi Juzuu 30 na akatunukiwa Sh60,000 na kifurushi cha kuenda kuhiji Mecca.

Aliyeshikilia nafasi ya pili ni Twahir Ali ambaye alikuwa mshiriki wa kibinafsi na akatuzwa Sh50,000. Aliyemaliza katika nafasi ya tatu ni Abdilatif Abdi Mirad aliyepokezwa Sh40,000.

Mshindi wa kuhifadhi Juzuu 20 alikuwa Abdulswamad Alwi–mshiriki wa kibinafsi– aliyetuzwa Sh40,000. Ayub Hussein kutoka jiji kuu Nairobi alikuwa wa pili katika kitengo hicho ambapo alipata Sh30,000 hali Ayman Mohamed wa Lucky Summer pia jijini Nairobi akawa wa tatu na kutuzwa Sh20,000.

Washindi wa kuhifadhi Juzuu 10 walikuwa ni Abdulrazak Ahmed, Banin – Nairobi (Sh15,000) akifuatwa na Hamza Muhamed (Sh10,000) naye Abdulhamid Adam, Banin- Nairobi (Sh7,000) akifunga tatu bora.

Washindi wa Juzuu tano walikuwa Abdulkheri Shiekh, Congo Boys-Markaz Nur (Sh10,000), Swaleh Nurdin, Dar Swaleh Mombasa (Sh10,000) na Marwan Shamun, Hamamatul-Quram Mombasa (Sh5,000).

Katika kitengo cha kimataifa cha kuhifadhi Juzuu 30, mshindi alikuwa Abdilatif Abdi Mirad wa Kenya aliyepokea Sh80,000 pamoja na tuzo ya simu aina ya iPhone 11, huku nafasi ya pili ikimwendea Muhammad Khamis kutoka visiwani Zanzibar aliyepata Sh60,000. Naye Twahir Ali wa Kenya alikamata nafasi ya tatu na kupata Sh40,000.