Habari za Kitaifa

Tukio adimu Ramadhani na Kwaresma zikiwasili wakati mmoja na kukoleza imani, upendo

Na STEPHEN ODUOR March 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KADRI mwangaza wa alfajiri unavyotokea, dunia huamka kutoka usingizini na waumini wa dini mbili—Ukristo na Uislamu—huamka kwa unyenyekevu.

Huu ni mwezi ambapo waumini wa dini hizi mbili, ingawa na imani tofauti, wanazingatia ibada muhimu: Kwaresma kwa Wakristo na Ramadhani kwa Waislamu.

“Kwa mara ya kwanza, dini hizi mbili zimeungana katika kufunga na kusali. Labda imetokea hapo awali, lakini kwangu mimi, hii ni mara ya kwanza kushuhudia wakati mzuri kama huu katika dini,” anasema Sheikh Ali Pama.

Katika kipindi hiki cha Kwaresma kwa Wakristo na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wa Kiislamu, waumini wa dini zote mbili wanashiriki ibada ya kufunga, sala, na tafakari.

Ingawa kuna tofauti za kiitikadi kati ya safari hizi mbili za kiroho, matendo yao huunda daraja la uzoefu wa pamoja, fursa ya umoja inayovuka mipaka ya kidini.Katika miji na vijiji kote nchini, alfajiri inakaribishwa kwa sauti ya ibada.

Kwa Waislamu, chakula cha kabla ya alfajiri, Suhoor, ni wakati mtakatifu. Waumini huamka kabla ya jua kuchomoza ili kula kabla ya kuanza siku ya kufunga.Kwa Wakristo, saa za mapema za asubuhi wakati wa Kwaresma, hasa siku za kufunga, hutumiwa katika sala na kutafakari.Dini zote mbili zinakumbatia mwanzo wa siku kwa mtazamo wa kiroho.

“Katika siku za kawaida, sijawahi kuona Wakristo wakihudhuria sala za alfajiri, lakini katika msimu huu, nawaona kwa wingi wakielekea kanisani saa kumi na moja asubuhi na kurejea nyumbani kujiandaa kwa kazi, jambo linalofurahisha roho yangu,” anasema Sheikh Pama.

Kadri siku inavyoendelea, kufunga kunabaki kuwa tendo kuu la ibada kwa dini zote mbili.Waislamu hujizuia kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi jua linapozama.

Kwa upande mwingine, Wakristo wanaoshiriki Kwaresma wanaweza kufunga kwa njia tofauti, kama vile kuacha kula baadhi ya mlo, kujinyima anasa fulani, au kujitolea kwa matendo ya hisani na kutafakari.

“Kinachounganisha ibada hizi ni nidhamu ya kujinyima na nguvu ya kiroho inayotokana na hilo. Tunawaomba Wakristo wajitolee zaidi, wajinyime matamanio yao kwa ajili ya wahitaji,” anasema Robert Mkolwe, Mwenyekiti wa Muungano wa Dini, Tana River.

Kwa Wakristo na Waislamu, kufunga si suala la kujinyima tu, bali ni njia ya kumkaribia Mungu kwa kujitolea.Jioni inapofika, jua likizama, roho ya umoja na mshikamano inajidhihirisha tena.

Kufungua saumu, iwe ni Iftar kwa Waislamu au kumaliza siku ya kujizuia kula kwa Wakristo wanaoshiriki Kwaresma, ni wakati wa kukusanyika pamoja.

Katika baadhi ya jamii nchini, chakula cha jioni cha pamoja kati ya waumini wa dini tofauti kimekuwa alama ya mshikamano, ambapo Wakristo na Waislamu huketi pamoja, wakiunganishwa na uzoefu wao wa kufunga.

“Katika msimu kama huu, tunajali kila mmoja. Baada ya kipindi kigumu cha kuvumilia na nidhamu ya imani, jambo bora zaidi ni kuwa familia moja,” anasema Halima Salat, mwalimu wa Madrasa.Katika baadhi ya vitongoji vya Kaunti ya Tana River, kwa mfano, ni kawaida kuona familia za dini tofauti zikialikana kufuturu pamoja.

Chakula cha jadi cha Iftar cha Waislamu mara nyingi hugawanywa na majirani wao Wakristo, huku familia za Kikristo zinazoshiriki Kwaresma zikiwakaribisha marafiki wao Waislamu.

Taswira ya wanaume na wanawake wa dini tofauti wakikusanyika meza moja, wakila na kusali pamoja, ni ushahidi wa nguvu ya imani katika kukuza jamii yenye mshikamano.

Miezi hii pia inaangaziwa na matendo ya hisani, jambo jingine linalounganisha dini hizi mbili.Dini zote mbili hupata nguvu na faraja katika nyakati hizi za kuungana na Mungu na wao kwa wao.

“Kwaresima na Ramadhani zote mbili zinahitaji waumini watafakari, watubu, na wafufue upya ahadi yao kwa lengo kuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kila mmoja anashinda dhambi na vishawishi vya dhambi kwa kutafuta utakaso,” anasema Askofu Richard Yaro wa Kanisa la Methodist Kenya