• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Waislamu watakiwa kusubiri tangazo la Kadhi Mkuu kuhusu Ramadhan

Waislamu watakiwa kusubiri tangazo la Kadhi Mkuu kuhusu Ramadhan

NA CECIL ODONGO

KADHI Mkuu Abdulhalim Hussein Jumapili, Machi 10, 2024 alitoa wito kwa Waislamu kusubiri tangazo lake pekee kabla ya kuanza kufunga kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Sheikh Abdulhalim kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali alisema kuwa si jambo jema kidini kwa Waislamu kutofautiana kila mwaka kuhusu siku ya kuanza na kukamilika kwa mfungo wa Ramadhan.

Kiongozi huyo wa kidini hasa aliwakabili wale ambao wamekuwa wakifuata Saudi Arabia ambako mwezi huandama kabla ya Kenya, akisema wao ndio wamekuwa wakiwachanganya Waislamu.

“Tumewekwa mamlakani kutoa mwongozo kwa Waislamu kuhusiana na kuonekana kwa mwaandamo wa mwezi kabla ya Ramadhan na kukamilika kwake. Kwa hivyo, Waislamu wote wanastahili kusubiri mwelekeo kutoka kwetu kama viongozi wao kuhusu masuala ya dini,” akasema Sheikh Abdulhalim.

“Tuko maeneo tofauti ya kijiografia na Saudi Arabia kwa hivyo Waislamu wanastahili kufuata kile ambacho sisi tuliopo mamlakani tunasema. Tukiuona mwezi, basi tutatangaza kuwa mfungo wa Ramadhan umeanza,” akaongeza.

Ufalme wa Waislamu Saudi Arabia Jumapili ulianza mchakato wa kutafuta mwezi japo Kadhi Mkuu anasema kuwa Kenya watauanza Jumatatu jioni katika afisi zake jijini Mombasa.

Kama mwezi utaonekana Saudia mnamo Jumapili baada ya maombi ya jioni, basi Waislamu huko wataanza kufunga mnamo Jumatatu.

Hali kama hii ndiyo imekuwa ikizua mchanganyiko baadhi ya Waislamu kutoka Kenya wakianza kufunga nao.

Iwapo mwezi hautaonekana Suadia mnamo Jumapili basi utasakwa tena Jumatatu kisha Waislamu huko waanze kufunga Jumanne.

Haya yanajiri wakati ambapo Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) kupitia Mwenyekiti wake Hassan Ole Naado wametoa wito kwa Waislamu wazingatie umoja na suala la mwandamo wa mwezi halifai kuwagawanya.

“Baraza linatambua huwa kuna tofauti kuhusu tarehe ya kuanza kwa Ramadhan kulingana na mwandamo wa mwezi. Licha ya tofauti hizi Supkem inatoa wito kwa Waislamu wasalie wameungana,” akasema Bw Naado.

Wakati huo huo, uongozi wa Supkem umeshukuru utawala wa Rais William Ruto kwa mchango wake wa Iftar kwa umma wa Kiislamu kipindi cha Ramadhan.

Pia umeshukuru serikali kwa kuondoa ushuru katika shehena za tende zitakazokuwa zikiletwa hapa nchini kipindi cha Ramadhan.

“Tunatoa wito kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) ihakikishe kuwa agizo la Rais kuhusu tende linatekelezwa,” akaongeza Bw Naado katika kikao na wanahabari Nairobi.

Supkem pia imemshukuru Rais kwa kumteua Aden Mohamed kama Balozi wa Jeddah Saudi Arabia, akielezea Imani yake kuwa atasaidia Wakenya wanaoenda Hajj na Umrah.

 

  • Tags

You can share this post!

Ndondi: Friza apoteza kushiriki Olimpiki, Kenya Ikirudi...

Vyama 48 vya kisiasa kugawana Sh2 bilioni

T L