Waititu bado hajapata benki ya kumdhamini ili atoke jela
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, bado hajapata benki ya kumdhamini ili aachiliwe huru kwa dhamana kuhusiana na kesi ya ufisadi inayohusu kandarasi ya ujenzi wa barabara ya thamani ya Sh588 milioni, Mahakama Kuu jijini Nairobi ilielezwa Jumatano.
Wakili wake, Bw Chris Mutuku, aliambia mahakama kuwa licha ya juhudi, mwanasiasa huyo aliyefungwa bado hajapata benki ya kumpa dhamana ya Sh53.5 milioni inayohitajika na Idara ya Mahakama.
Kutokana na ukosefu huo wa mdhamini, wakili huyo aliomba mahakama ipunguze masharti ya dhamana hiyo kutoka dhamana ya benki ya Sh53.5 milioni hadi dhamana ya pesa taslimu ya Sh20 milioni, akitaja ugumu wa kupata mdhamini na hali mbaya ya kiafya ya Waititu.
Hata hivyo, hakufafanua sababu za kutopata mdhamini kwa zaidi ya miezi miwili, ingawa benki kawaida huhitaji dhamana ya mali au tathmini ya hatari kabla ya kutoa dhamana kama hiyo.
Wakili huyo aliambia mahakama kuwa mteja wake, ambaye alihukumiwa Februari mwaka huu kifungo cha miaka 12 jela au kulipa faini ya Sh53.5 milioni, ni mgonjwa na anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).
Anataka mahakama ibadilishe agizo lililotolewa Julai 20, 2025, ambapo mahakama ilimruhusu Waititu kupata dhamana ya muda kusubiri uamuzi wa rufaa yake kwa “sharti kwamba atawasilisha dhamana ya benki inayokubalika kwa faini yote ya Sh53.5 milioni kwa niaba ya mahakama.”
Dhamana ya benki ni hati ya kifedha ambapo benki huahidi kulipa kiasi fulani cha pesa kwa mhusika endapo mteja wa benki atashindwa majukumu yake ya mkataba na katika kesi hii ni ikiwa Waititu atashindwa kuhudhuria vikao vya kesi.
Dhamana hiyo humhakikishia mahakama kuwa endapo mshukiwa atakiuka masharti, hasara itafidiwa. Inafanya kazi kama aina ya amana ya usalama.
Wakati rufaa hiyo ilipoitwa mbele ya Jaji Lucy Njuguna kwa ajili ya kusikilizwa kabla ya kesi kuanza rasmi, Wakili Mutuku alisema kuwa ingawa bado hawajapata mdhamini, Waititu si mtu wa kutoroka.
Aliomba mahakama ipunguze masharti iliyotoa Julai 2025.
“Tumeshindwa kupata dhamana ya benki kama ilivyoamriwa na mahakama, na ndiyo maana mteja wetu bado yuko rumande. Amepewa nafasi ya kutibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” wakili huyo aliambia Jaji Njuguna aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo katika Kitengo cha Ufisadi.
Waititu alilazwa hospitalini hapo Mei 2025 baada ya kuugua akiwa katika Gereza la Kamiti.
Hata hivyo, Jaji Njuguna alikataa ombi hilo la haraka lakini aliruhusu upande wa utetezi kuwasilisha tena ombi hilo wiki ijayo Jumatatu kesi hiyo itakapotajwa.
Alisema agizo la dhamana ya benki lilitokana na ombi la Waititu mwenyewe aliyedai angeweza kupata.