Wakazi, viongozi waomboleza kifo cha Naibu Gavana wa Lamu Raphael Ndung’u
WAKAZI wa Lamu wanaomboleza kifo cha cha Naibu Gavana, Raphael Munyua Ndung’u wakimumiminia sifa kedekede kwa kazi yake.
Rais William Ruto ni miongoni mwa waliotuma risala za rambirambi zao huku gavana wa Lamu, Issa Abdallah Timamy, akiwasihi wananchi wa Lamu kutumia kifo cha Naibu wake kuwa kigezo cha kuwaunganisha hata zaidi kama jamii.
Bw Ndung’u alifariki Ijumaa, September 6,2024 wakati akipokea matibabu kwenye hospitali ya Nairobi.
Kwenye ujumbe wake kwa vyombo vya habari, Bw Timamy alimtaja Bw Ndung’u kuwa kiongozi mkakamavu na mwadilifu ambaye alipigania sana umoja wa watu wa Lamu.
Bw Timamy alisema ili kumuenzi mwendazake, itakuwa vyema kwa wananchi na jamii nzima ya Lamu kuendeleza azma ambayo Bw Ndung’u aliipigania katika uhai wake, hasa umoja, maendeleo na maelewano.
‘Bw Ndung’u hakuwa Naibu wangu tu bali mchapa kazi mwenza, rafiki na ndugu. Wakati tunapoomboleza, hebu tuje pamoja kuyatafakari na kuyaendeleza yale ambayo marehemu amekuwa akiyapa kipaumbele wakati wa kuishi kwake hapa duniani ambayo ni umoja, maendeleo na maelewano,’ akasema Bw Timamy.
Viongozi wengine waliowasilisha rambirambi zao kwa wakazi wa Lamu kufuatia kuondokewa na Naibu huyo wa Gavana ni Gavana wa Mombasa na Naibu Kinara wa ODM, Abdullswamad Shariff Nassir aliyemtaja Bw Ndung’u kuwa kiongozi jasiri aliyeungana na viongozi wa Pwani katika kupigana vita dhidi ya tabia potovu kwa jamii, ikiwemo ulaji wa muguka na uraibu mwingine.
‘Ni bayana kwamba wananchi wa Lamu walikuwa na kiongozi wa maana aliyejikaza kutenda yaliyo mema, kusimama na haki na kufokea maovu katika jamii. Nawaoa pole Gavana Issa Timamy, ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wa Lamu Kwa jumla kwa kumpoteza Naibu Gavana Ndung’u,’ akasema Bw Abdullswamad.
Bw Ndung’u alizaliwa eneo la Umoja, tarafa ya Mpeketoni, Lamu Magharibi. Alisomea Shule ya Msingi ya Umoja kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Mpeketoni.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta alikosomea Hisabati ya Usanifu Majengo (Architectural Mathematics).
Amewahi kufanya kazi na mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya kiserikali hapa Kenya na pia nchi jirani ya Tanzania kabla ya kujiunga na siasa mnamo mwaka 2013, akiwa mgombea mwenza wa gavana wa zamani wa Lamu, Fahim Yasin Twaha.
Amewahi kuhudumu kama Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu.
Mnamo 2022, alivuka na kuwa mgombea mwenza wa gavana wa sasa, Issa Timamy, muungano uliomwezesha kumshinda Bw Twaha kwenye uchaguzi huo wa Agosti 9, 2022.
Bw Munyua ni baba wa watoto wawili.