• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wakazi wa Molo watoroka mafuriko

Wakazi wa Molo watoroka mafuriko

NA JOHN NJOROGE

TAKRIBAN familia 100 zinatafuta makao mbadala baada ya nyumba zao kujaa maji ya mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Alhamisi usiku katika mtaa wa Kaloleni ulioko mjini Molo, Kaunti ya Nakuru.

Taifa Leo lilipofika eneo hilo, wapangaji walikuwa wanabeba vitu vya nyumbani vikiwemo vitanda na masofa, vyombo vya kutumika jikoni na mali zao za kibinafsi.

Aidha, waathiriwa wanahamisha mifugo yao na kupeleka katika maeneo salama kwa hofu ya kuathiriwa na mafuriko zaidi.

Kwa kutumia bodaboda, mikokoteni inayovutwa na punda na malori, walioathirika walionekana Ijumaa wakihamisha mali zao kwa kuhofia madhara zaidi huku mvua ikiendelea kunyesha katika eneo hilo.

Bi Beth Wangui, mkazi wa Kaloleni, alisema waliamka usiku wa manane na kukesha hadi alfajiri kwani nyumba zao zililoa maji yaliyotokana na mvua kubwa usiku mkuu.

Wakazi wa Kaloleni, Molo, Kaunti ya Nakuru wahama kutoka kwa makazi yao kufuatia mafuriko. PICHA | JOHN NJOROGE

“Mafuriko hayo yalitokea katika maeneo ya nyanda za juu na kuingia kwa nyumba zetu na ikalazimu mimi na familia yangu kuhamia maeneo yaliyo salama zaidi,” akasema Bi Wangui.

Ni baada ya msamaria mwema kujitolea kuwapa sehemu ya kuweka vitu ambavyo wameviokoa kwa siku chache.

Mkazi huyo alisema mvua iliathiri kila kitu ndani ya nyumba yake ikiwa ni pamoja na nguo, vyakula na vitu vingine.

Bi Wangui aliongeza kuwa baadhi ya kuku wake walisombwa na maji.

Alitoa wito kwa wakazi wengine ambao wameathiriwa na mafuriko hayo kuhama badala ya kusubiri mabaya yatokee, hasa wale wanaoishi karibu na mto.

Alisema si mara ya kwanza wao kuathirika na mafuriko katika eneo hilo.

Alibainisha kuwa mwaka 2023, tukio kama hilo lilitokea na kuwaacha wakazi wakikadiria hasara.

Mkazi mwingine, Bi Margaret Masobo, alisema licha ya nyumba yake kujaa maji, hataondoka eneo hilo kwa kuwa hana pa kuenda.

Hii ni licha ya serikali kutishia kuwahamisha watu kama hao kwa lazima.

“Ni wito wangu kwa serikali ya kaunti kuja kutusaidia na kuondoa tope katika maeneo ambayo yamezibwa kufuatia mvua inayoendelea kunyesha. Huenda tukakumbwa na maafa zaidi katika eneo hili ikiwa mvua itaendelea kunyesha,” alisema Bi Masobo na kuongeza kuwa njia za kupitishia maji zimezuiwa, hii ikiwa ni mojawapo ya changamoto kubwa hasa mvua inaponyesha.

Diwani wa eneo hilo Bw Joseph Ngware, alisema takriban familia 200 zimeathiriwa na mafuriko hayo na kuwataka wale ambao hawajahamia sehemu salama kufanya hivyo mara moja.

“Tunatoa wito kwa wale wanaoishi karibu na mito, nyanda za chini au kando ya maeneo chepechepe kuhama haraka iwezekanavyo hadi maeneo salama ili kuzuia matukio kama haya katika siku zijazo.

Alisema wakati huo huo, hatua zinaendelea ili kuwasaidia wale walioathirika na kuwataka wasisubiri mafuriko kufika bali wahame ili kuokoa maisha na mali yao.

Haya yanajiri huku idadi ya waliopoteza maisha yao kufuatia mafuriko eneo la Mai Mahiu ikifika 55 baada ya miili mitatu zaidi kupatikana Ijumaa jioni.

Afisa Mkuu wa Afya ya Umma katika Kaunti ya Nakuru Joyce Ncece amethibitisha.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kashmir Lamu: Makao makuu ya kuharibu mihadarati

Mwaniaji aliyetishia kumuua diwani Makueni atupwa jela...

T L