• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Wakenya 4,500 kutekeleza ibada ya Hajj 2024

Wakenya 4,500 kutekeleza ibada ya Hajj 2024

NA FARHIYA HUSSEIN

WAKENYA 4,500 watatekeleza ibada ya Hajj nchini Saudi Arabia mwaka 2024, kulingana na Baraza Kuu la Waislamu Nchini (Supkem).

Wasimamizi wa maandalizi ya safari za Hajj kutoka Kenya chini ya mwavuli wa Supkem, walitia saini itifaki za msimu wa Hajj wa 2024 na Wizara ya Masuala ya Hajj na Umrah ya Ufalme wa Saudi Arabia huko Jeddah.

Makubaliano hayo yanaainisha ahadi na wajibu wa wahusika katika makubaliano hayo.

Wakuu kutoka Kenya waliongozwa na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Supkem, Al-Hajj Hassan Ole Naado, na kujumuisha wajumbe wengine.

Makubaliano hayo yalitiwa saini na Naibu Waziri wa Masuala ya Hajj na Umra–kwa niaba ya Ufalme wa Saudi Arabia–na Al-Hajj Hassan Ole Naado.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na washiriki wakuu, akiwemo Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Kenya Khalid Al-Salman na Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Masuala ya Hajj na Umrah Dkt Badr Al-Solami.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Masuala ya Hajj na Umrah Dkt Abdul Fattah Suleiman Al-Mashat, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia muda uliowekwa katika maandalizi ya msimu wa hajj 2024.

Aliuhimiza ujumbe wa Kenya kukamilisha mikataba iliyosalia na watoaji wa huduma ambazo ni pamoja na nyumba za maeneo ya Mecca na Madina, milo katika miji mitakatifu, na usafiri.

“Ufalme wa Saudi Arabia umejitolea kutoa huduma nzuri kwa mahujaji kutoka kote ulimwenguni ili kuwawezesha kutekeleza ibada ya hajj kwa raha,” alisema Dkt Al-Mashat.

Kwa upande wake, Bw Ole Naado aliishukuru Wizara ya Masuala ya Hajj na Umrah kwa juhudi zao zinazoendelea katika kuboresha huduma na kuratibu shughuli zinazohusiana na Hajj duniani kote.

Bw Ole Naado alithibitisha kuwa Wakenya 4,500 watatekeleza ibada ya Hajj mwaka 2024 na kuahidi kushirikiana kikamilifu na Wizara ya Hajj na Masuala ya Umrah ya Ufalme wa Saudi Arabia.

Pia alisema kuwa yeye na ujumbe wake pamoja na wasimamizi wa Hajj, Kenya, watahudhuria Kongamano kuhusu Hajj 2024 huko mjini Jeddah, Saudi Arabia. Kongamano hilo litahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 129 na litaanza Jumatatu, Februari 8, 2024.

Tarehe za hajj ni baina ya Juni 14, 2024, na Juni 19, 2024.

Makubaliano ya kufanikisha ziara ya mahujaji 4,500 yalitiwa saini na Naibu Waziri wa Masuala ya Hajj na Umrah Dkt Abdul Fattah Suleiman Al-Mashat–kwa niaba ya Ufalme wa Saudi Arabia–na Mwenyekiti wa Supkem Al-Hajj Hassan Ole Naado. PICHA | HISANI
  • Tags

You can share this post!

Kioni: Uhuru ndiye ‘kingpin’ wa Mt Kenya hadi...

Nitaanza kutoka na vibenten kwa jinsi mnavyonisema, atishia...

T L