Wakenya kukopa Sh4 milioni kutoka hazina ya nyumba kujenga mashambani
WAKENYA sasa wanaweza kukopa hadi Sh4 milioni kutoka kwa Hazina ya Nyumba za Gharama Nafuu (AHF) kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama ndogo mashambani baada ya bunge kupitisha kanuni mpya.
Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Sheria Mbadala imepitisha Kanuni kuhusu Nyumba za Gharama Nafuu ya 2025 zilizotayarishwa na Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji inayoongozwa na Waziri Alice Wahome.
“Baada ya kuchambua Kanuni kuhusu Nyumba za Gharama Nafuu za 2025 (Notisi ya Kisheria Nambari 114) kamati hii inapendekeza kuwa bunge lipitishe Kanuni hizo,” mwenyekiti wa kamati hiyo Samuel Chepkonga akasema kwenye ripoti.
Sheria za Bunge zinahitaji kwamba baada ya Kamati kuhusu Sheria Mbadala kuwasilisha ripoti yake ya kuidhinisha kanuni kielelezo, Karani wa Bunge la Kitaifa ataijulisha, kwa maandishi, asasi iliyotunga kanuni hizo kwamba izichapishe kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.
Hata hivyo, Wakenya ambao watataka kuomba mikopo hiyo kutoka kwa Bodi ya Hazina ya Nyumba za Gharama Nafuu watahitajika kutimiza mahitaji magumu ili kupata pesa hizo.
“Mtu atatuma maombi ya mkopo wa kujenga nyumba maeneo ya mashambani ikiwa amekuwa akitoa mchango kwa hiari katika hazina hiyo na hajawahi kutengewa nyumba ya gharama nafuu. Pia atahitajika kutimiza masharti ya uhitimu yaliyoko katika kanuni nambari 3,” kulingana na kanuni hizo.
“Kiwango cha mkopo kitakachotolewa kwa yule ambaye atafaulu hakitazidi Sh4 milioni,” kanuni hizo zinaongeza.
Kanuni hizo mpya zinaeleza kuwa mtu aliyetimiza masharti hitajika anaweza kuwasilisha maombi yake, ya mkopo, kielektroniki kwa bodi hiyo.
Hata hivyo, mtu kama huyo atahitajika kuwasilisha nakala ya kibali kutoka kwa Waziri wa Ardhi katika kaunti yake, ripoti ya tathmini ya ardhi ambako atajengea nyumba hiyo, ripoti iliyotolewa na mtaalamu aliyesajiliwa kulingana na Sheria ya Wataalamu wa Kukadiria Thamani ya Ardhi na Taarifa kuhusu Gharama ya Ujenzi iliyotayarishwa na Msanifu Mijengo aliyesajiliwa rasmi.
Wanaoomba mikopo pia watahitajika kuwasilisha kwa bodi hiyo nakala ya hatimiliki ya ardhi hiyo iliyosajiliwa kwa jina lake.
Aidha, wanaotaka mikopo watahitajika kuwasilisha hati rasmi inayoonyesha kuwa mkopo huo utatumika kwa ujenzi wa nyumba ya gharama nafuu pekee.
“Wakati wa kuchambua maombi ya mikopo, bodi hiyo inaweza kuchunguza ikiwa aliyewasilisha ombi husika amekuwa akiwasilisha michango ya hiari katika Hazina hiyo ya Nyumba Gharama Nafuu.
“Aidha, Bodi itatathmini iwapo aliyeomba mkopo huo anao uwezo wa kuulipa kiasi alichoomba,” kanuni hizo zinaeleza.
“Endapo ombi la mkopo litaidhinishwa, Bodi itaweka mkataba wa makubaliana na mhusika na kuwasilisha pesa hizo kwa akaunti ya mtu huyo kulingana na makubaliano hayo.
“Hii ni baada ya aliyetuma ombi kulipa ada hitajika kwa bodi hiyo na kuchukua bima kwa mkopo huo,” kanuni hizo zinaongeza.
Mchango wa hiari ni tofauti na makato ya kila mwezi kwa kila mfanyakazi na mwajiri wake.
Kwa sasa serikali hukata asilimia 1.5 kutoka kwa mshahara wa walioajiriwa nao waajiri hulipa kiasi sawa na hicho kwa kila mfanyakazi wao.
Mbali na ujenzi wa mashambani, mnamo Juni 1, 2025, Rais William Ruto alitangaza mipango ya kuwawezesha watu walioajiriwa, ambao wanakatwa makato hayo, kupata mikopo ya riba nafuu ili wanunue nyumba za bei nafuu.