Habari za Kitaifa

Wakenya kupumua kiasi mafuta yakishuka bei  

January 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

NI afueni kidogo tena kwa Wakenya baada ya serikali kupunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa angalau Sh5 kwa lita.

Kulingana na bei mpya iliyotangazwa Jumapili, Januari 14, 2024 na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) bei ya petroli na dizeli imepungua kwa Sh5 huku ile ya mafuta taa ikishuka kwa Sh4 na senti 82 kwa lita.

Hii ina maana kuwa petroli itauzwa Sh207.36 jijini Nairobi kutoka Sh212.36 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh196.47 kuanzia Januari 15, 2024 hadi usiku wa Februari 15, 2024.

Nayo mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh194.23 kutoka Sh199.05 kwa lita jijini Nairobi na viunga vyake ndani ya siku 30 zijazo.

“Kulingana na Sehemu ya 101 (y) ya Sheria ya Petroli ya 2019 na Notisi ya Kisheria nambari 192 ya 2022, EPRA imekadiria bei ya rejareja ya bidhaa za mafuta zitakazotumika kuanzia Januari 15 hadi Februari 14, 2024,” EPRA ikasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

“Katika kipindi hicho bei inayoruhusiwa ya Petroli, Dizeli na Mafuta taa zimepunguzwa kwa kiwango cha Sh5, Sh5 na Sh4.82 kwa lita, mtawalia”.

EPRA ilisema bei hizo mpya zinajumuisha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16 kulingana na hitaji la Sheria ya Fedha ya 2023.

Hii ni mara ya pili kwa bei ya mafuta kushuka kwa mwezi wa pili kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.

Bei ya Mafuta yasiyosafishwa imepungua kwa asilimia 10 katika mwaka wa 2023, kiwango ambacho ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Desemba 2023 EPRA ilipunguza bei ya petroli kwa Sh5, bei ya dizeli kwa Sh2 na ile ya mafuta taa kwa Sh4.01 kwa lita.

Hata hivyo, katika mwezi huo kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipuuzilia mbali punguzo hilo akisisitiza kuwa serikali ilipaswa kupunguza bei hiyo kwa kiwango cha kati ya Sh45 na Sh50 kwa lita.