• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Wakenya sita wauawa na Al-Shabaab wakichuuza bidhaa nchini Somalia

Wakenya sita wauawa na Al-Shabaab wakichuuza bidhaa nchini Somalia

NA CHARLES WASONGA

WAFANYABIASHARA sita Wakenya wameuwa katika mji wa Dhobley ulioko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Garissa John Samburumo alisema kuwa sita hao ni miongoni mwa wachuuzi ambao huvuka mpaka kila siku kwenda kufungua biashara zao katika mji huo.

“Kisa hicho kilitokea Ijumaa mwendo wa saa moja na robo. Walishambuliwa kwa risasi na wapiganaji waliokuwa wakisafiri kwa gari aina ya Probox,” akasema Bw Samburumo.

Aliongeza kuwa wanne walifariki papo hapo ilhali wengine wawili walipata majeraha na kuaga dunia walipokuwa wakipokea matibabu katika kituo cha afya kilichoko karibu.

Walioshuhudia kisa hicho waliripotiwa wakisema kuwa wavamizi hao walikuwa wamefunika nyuso zao na hivyo wanashukiwa kuwa wafuasi wa kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab.

Uchunguzi kuhusu kisa hicho unaendelea japo maafisa wa poliis wanashuku kuwa shambulio hilo lilichochewa kidini.

Inasemekana kuwa waliouawa ni waumini wa dini ya Kikristo, ambao ni wachache katika eneo hilo ambalo watu wengi ni Waislamu.

Inadaiwa pia kuwa wafanyabiashara hao walituhumiwa kueneza dini ya Kikristo mjini Dhobley.

Shambulio hilo limeibua hofu na hasira miongoni mwa wafanyabiashara raia wa Kenya ambao hutegemea biashara ya uchuuzi kujipatia riziki.

  • Tags

You can share this post!

Gavana aonya wanaotoza chekechea karo

Wavinya akemea ufisadi akibeba msalaba Ijumaa Njema ya...

T L