Wakenya waliohamia Amerika waingia hofu uchaguzi ukiwadia
HUKU Amerika ikielekea kwenye siku ya uchaguzi Jumanne, Novemba 5, 2024, Wakenya wanaoishi nchini humo wameelezea wasiwasi wao kuhusu usalama na kuishi kwao hasa ikiwa mgombea wa Republican, Donald Trump, atashinda.
Trump anayeng’ang’ana kuwabandua wana Democrat na kurejea Ikulu ya White House, ametishia kuwafurusha wahamiaji ikiwa atambwaga Kamala Harris.
Mpango wa Trump unajumuisha ajenda ya kuwapokonya wahamiaji haki yao kikatiba ya uraia na kukatiza mpango wa kuunganisha familia, unaoruhusu wakazi wa kudumu na raia waliobadilishiwa uraia kutuma maombi ya jamaa zao kujiunga nao Amerika.
Kisa cha ufyatulianaji risasi majuzi katika jimbo la Minneapolis kimezidisha hofu miongoni mwa Wakenya wanaoamini urais wa Trump, ikiwa utatimia, utaanzisha sera inayopinga wahamiaji na kuwafurusha raia wengi wa kigeni kutoka nchini humo.
Bw Davis Moturi, aliyepigwa risasi na kujeruhiwa Minnesota, alikuwa ameandikisha ripoti karibu 20 kwa polisi wa Minneapolis kwamba jirani mzungu alikuwa anajaribu kumuua kwa sababu ya chuki ya rangi ya ngozi, lakini walinda usalama wakakosa kuchukua hatua na kumpa ulinzi.
Huku taharuki ikizidi kutanda kisiasa na kuhusu ubaguzi wa rangi, dhana kuhusu wahamiaji imewaweka wahamiaji Wakenya hatarini huku wengi wakijiandaa kwa nyakati ngumu siku za usoni.
Walipokabiliwa na vyombo vya habari na viongozi eneo hilo kuhusu ni kwa nini walikosa kumlinda raia huyo wa Amerika mwenye asili ya Kenya kabla ya jirani yake anayedaiwa kumpiga risasi, polisi walisema walihofia maisha yao na hawakutaka kumhatarisha yeyote.
Walipoulizwa ni kwa nini iliwachukua wiki moja kumkamata mshukiwa, Mkuu wa Polisi Minneapolis, Brian O’Hara, alijibu “Uwezekano wa makabiliano ya kujihami ambapo huenda tukalazimika kutumia nguvu kupita kiasi na mshukiwa katika kisa hiki ni wa juu. Hatutavunja mlango, kufyatua risasi na kujiweka katika hali kama hiyo.”
Wakizungumza na Taifa Leo, viongozi wa jamii ya Wakenya, Amerika wakiongozwa na Wakili Henry Ongeri, waliwasihi Wakenya wanaoishi Amerika wasihofishwe na vitisho vya ubaguzi wa rangi kwa sababu wamelindwa kikatiba kutokana na hatua zinazokiuka sheria.