Wakenya waliokaidi onyo kusafiri Lebanon wateseka
WAKENYA bado wanaendelea kusafiri Lebanon kutafuta ajira licha ya serikali kupiga marufuku safari katika nchi hiyo.
Katibu katika idara ya Masuala ya Kigeni, Roseline Njogu, aliambia Taifa Leo kuwa marufuku ya kusafiri Lebanon imekuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Tumewashauri Wakenya mara kwa mara kutosafiri Lebanon kutafuta kazi wakati huu. Tathmini yetu imeonyesha kuwa Lebanon si mahali salama kwa Wakenya kwa sababu hatuna makubaliano rasmi ambayo yanahakikisha haki zao au kuhakikisha wanapata huduma za kibalozi,” Bi Njogu alieleza.
Serikali imewashauri Wakenya kuahirisha safari ya kwenda katika baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati, zikiwemo Lebanon na Palestina hadi hali ya utulivu itakaporejea kutokana na mzozo unaoendelea.
Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi alionya dhidi ya kusafiri maeneo haya, akibainisha kuwa hali nchini Lebanon imezidi kuwa mbaya na kwamba, imeathiri takriban Wakenya 26,000 wanaofanya kazi huko kwa sasa.
Mzozo huo ulizidi Oktoba 2023 wakati Israeli iliposhambuliwa na Hamas. Mwezi uliopita, Katibu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo alisema Kenya inahitaji angalau Sh2 bilioni ili kuwaleta Wakenya 7,200 walio Lebanon nchini.
IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO