Wakenya wanaoteswa Saudi Arabia walipitia mlango wa nyuma, Waziri asema
Na WINNIE ATIENO
WAKENYA ambao wanaendelea kuhangaika nchini Saudi Arabia walisafiri bila stakabadhi za kuajiriwa, serikali imesema.
Waziri wa Leba Florence Bore anasema hata baada ya Kenya kuweka mikataba na nchi kadhaa za Kiarabu, baadhi ya Wakenya husafiri nchi hizo bila stakabadhi kamili.
“Tumeweka mikataba na nchi nne na bado tunaendelea na hizo zingine. Kwenye mikataba yetu huwa tunaangalia maslahi ya watu wetu. Mtu aishi salama na mwajiri wake, alipwe vizuri, afanye kazi kwa muda unaofaa na kandarasi inasemaje kuhusu ajira hizo,” alisema Bi Bore.
Alitaja maelewano kati ya Kenya na Saudi Arabia, hasa kwa wafanyikazi wa nyumbani.
“Shida tunayoona kule Saudi Arabia ni sababu walisafiri bila stakabadhi. Walisafiri kama wageni wakitumia visa ya wageni ambayo inaisha baada ya miezi mitatu. Mkenya akisafiri kama mtalii, baada ya miezi mitatu shida zinaanza kumwandama sababu alisafiri bila stakabadhi,” aliongeza.
Bi Bore aliwasihi Wakenya wafasiri Uarabuni wakitumia kandarasi ambayo itawaruhusu kufanya kazi kwa miaka miwili au mitatu.
Akiongea kwenye mahojiano na runinga moja Ijumaa, Bi Bore alisema Kenya inanuia kuweka mkataba na Saudi Arabia kwa wafanyakazi wataalam kama vile benki.
Waziri huyo alisema umuhimu wa mkataba unamlinda mfanyakazi anaposafiri nchi za Uarabuni.
Alisema wafanyakazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wanapofika kwa mwajiri wao wanapewa majukumu mengi.
“Wanapewa kazi nyingi, badala ya kwenda kufanya kazi nyumba moja anapelekwa nyumba zingine 10 anatumiwa na familia hiyo na pesa ni kidogo. Niligundua pia kuna Wakenya ambao wanasafiri wakitumia maajenti ambao hawajasajiliwa na serikali,” akasema waziri huyo.
Bi Bore alisema Mkenya anaposafiri kwa kutumia maajenti ghushi wanakosa watetezi na kubakia kuhangaika.
Alisema hivi majuzi alisafiri Saudi Arabia na kushuhudia mahangaiko ya wakazi.
Alitoa mfano ambapo alikutana na Wakenya karibia 300 wamehifadhiwa kwenye wa kituo kimoja wakisubiri kutengenezewa stakabadhi halali ili warudi Kenya.
Bi Bore alisema Wakenya pia husafiri nchi hizo wakisaka ajira bila ujuzi wala stakabadhi za kuonyesha utaalamu.
Hata hivyo, alisema serikali imeanza kukaza kamba kuhakikisha Wakenya wanaosafiri wanapewa mafunzo kuhusu nidhamu, umuhimu wa kufanya kazi wa kutumia mashini na desturi za Waarabu.
“Katika uwanja wa kimataifa wa ndege ya Jomo Kenyatta tumeweka deski ambayo inachukua idadi ya wafanyakazi wanaosafiri kwenda ughaibuni, nchi wanakoenda na kufanya kazi gani,” alisema Bi Bore.
Hatua hii alisema itasaidia serikali kufuatilia raia wake ughaibuni.
“Wengi wao hatujui ni kina nani na wako wengi bila stakabadhi kwa hivyo wakipata shida hata ubalozi hawana takwimu zao,” akaeleza.
Alisema ipo haja ya Wakenya wanaosafiri ughaibuni kujua afisi ya ubalozi ili wakipata matatizo wanakimbia kwa usaidizi.