Wakenya wasakatonge wakaidi serikali, waishia kuwa watumwa Asia Kusini
WAKENYA bado wanakaidi onyo la serikali na kwenda kutafuta kazi katika nchi za Asia Kusini ambako wanageuzwa watumwa.
Ilani ya serikali mnamo Ijumaa, Agosti 16, ilifichua kwamba mamia ya Wakenya, na raia wengine wa Afrika Mashariki, wameshawishiwa kuingia Myanmar, Laos na Cambodia kufanya kazi kama walimu wa lugha ya Kiingereza, lakini wanaishia kuwa vibarua wanaolipwa mshahara duni katika mazingira magumu ya vitisho na hatari.
Onyo la hivi punde lilitoka kwa Ubalozi wa Kenya nchini Thailand baada ya Mkenya aliyekwama nchini humo kufariki akiwa hospitalini.
Serikali ilisema tatizo hilo limekuwa kubwa hasa baada ya waajiri kuwapa Wakenya wengine jukumu la kuwashawishi wananchi kujiunga nao kwa ahadi za uongo.
Ubalozi wa Kenya pia unasimamia huduma za kibalozi kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki,Thailand, Myanmar, Laos na Cambodia.
Ubalozi ulisema hivi majuzi ulishirikiana na wasimamizi wa nchi hizo kuokoa Wakenya takriban 140 na Waafrika raia wengine wa Afrika Mashariki.
Hii inaonyesha jinsi hali hiyo inazidi licha ya onyo kutolewa 2022 kuhusu matapeli wanaorai watu kuhamia nchi hizo.
“Licha ya onyo ya kina na kampeni za kuhamasisha raia, kuendelea kwa ulaghai huu kunasalia kuwa jambo la kutia wasiwasi,” Ubalozi uliandika kupitia barua.
“Kwa sasa, Ubalozi unawasaka Wakenya watatu ambao wametoweka nchini Myanmar, kazi ambayo imefanywa kuwa hatari sana kutokana na mzozo wa wenyewe kwa wenyewe unaoendelea na mitandao ya kihalifu katika eneo hilo,” Ubalozi uliongeza ukirejelea vita kati ya jeshi la Burma na waasi ambao wamefanya nchi kukosa utawala wa sheria.