• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 1:33 PM
Wakenya wataka bei ya gesi ipunguzwe baada ya stima kushuka  

Wakenya wataka bei ya gesi ipunguzwe baada ya stima kushuka  

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya Kampuni ya Umeme Kenya (KP) kupunguza bei ya umeme kwa kiwango kikubwa, ni mwisho wa safari ya vilio vingi ambavyo vimekuwa na Wakenya kwa muda mrefu.

Jumatatu, Aprili 16, 2024, kampuni hiyo ilitangaza kupunguza bei ya umeme kwa asilimia 13.

Kulingana na kampuni hiyo, gharama ya umeme itashuka kwa Sh3.44 kwa kila kipimo.

KP ilitaja hali hiyo kuchangiwa na kuimarika kwa thamani ya Shillingi dhidi ya Dola na sarafu nyingine za kigeni na kushuka kwa bei za mafuta.

Ikizingatiwa serikali pia imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta, Wakenya na wafanyabiashara waliozungumza na Taifa Dijitali, walitaja hali hiyo kuwa ya kuridhisha.

Walisema ni mwelekeo unaoashiria kwamba hatimaye, huenda gharama ya maisha ikaanza kushuka, na kuwaondolea Wakenya mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa za msingi, kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa tangu 2022.

“Imani yetu ni kuwa huu ndio utakuwa mwelekeo kuanzia sasa. Tuna matumaini makubwa,” akasema Bw James Murage, ambaye ni mkazi wa eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.

Licha ya kushuka kwa bei hizo, baadhi ya Wakenya walisema serikali sasa inafaa kuangazia bei ya gesi ya kupikia, kwani bado iko juu.

Wanasema kwamba kupungua kwa bei ya mafuta na umeme kunamaanisha kuwa hata bei ya gesi ya kupikia inafaa kushuka.

“Bei ya gesi iliongezeka sana mwezi uliopita. Kwa sasa, bei ya kujaza mtungi wa kilo 13 ni Sh3, 330 kiwastani. Hiyo ni bei ya juu sana. Kinaya ni kuwa, Rais William Ruto aliwaahidi Wakenya kwamba serikali itafanya kila iwezalo kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu,” asema Bi Monicah Makokha, ambaye ni mkazi wa Nairobi.

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi nao wanasema kuwa huu ni mwanzo mzuri kwamba hatimaye mikakati ya serikali kupunguza gharama ya maisha hatimaye imeanza kuzaa matunda.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Bw Tony Watima, anasema kuwa hatua ya kwanza kwa serikali au nchi yoyote kupunguza gharama ya maisha miongoni mwa raia wake ni kushusha bei ya mafuta na umeme.

“Bei za mafuta na umeme huwa zinaathiri karibu kila kitu katika nchi. Wakati bei za bidhaa hizo mbili zinapoenda juu, hilo humaanisha kuwa gharama ya maisha hupanda moja kwa moja. Wakati bei zake zinaposhuka chini, hilo linamaanisha kuwa gharama ya maisha itaanza kushuka. Hivyo, hii ni dalili nzuri,” akasema mdadisi huyo.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Bwanyenye adinda kufika kortini kujibu kesi ya wizi wa...

Wakenya kupata afueni zaidi matatu zikipanga kushusha bei ...

T L