Habari za Kitaifa

Wakili adai watayarishaji filamu waliokamatwa walilazimishwa kutia saini taarifa

Na MERCY SIMIYU May 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKILI wa watayarishaji filamu wanne wa Kenya waliokamatwa Ijumaa usiku na kuachiliwa bila mashtaka Jumamosi asubuhi, amelaumu polisi kwa kuwalazimisha wateja wake kutia saini taarifa bila kuwa na mawakili na kuchukua vifaa vyao bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Bw Ian Mutiso pia alidai kuwa kukamatwa na kuhojiwa kwao kulitokana na jaribio la kuhusisha wanne hao na makala ya BBC Africa Eye, Blood Parliament, ambayo yalihusisha polisi na mauaji ya waandamanaji katika majengo ya bunge mwaka jana.

Nicholas Gichuki, Brian Adagala, Mark Denver Karubiu na Chris Wamae walikamatwa Ijumaa usiku na kuzuiliwa katika vituo vya polisi vya Pangani na Muthaiga.

Wakili wao sasa anadai kuwa mahojiano na polisi yalionyesha walikuwa wakijaribu kuhusisha wateja wake na makala ya BBC Africa Eye: Blood Parliament.

“Baada ya kukagua kitabu cha matukio ilibainika kuwa polisi walikusudia kuwashtaki kwa kuchapisha taarifa za uongo. Aidha, ilionekana kuwa polisi walichukua vifaa vyao kupitia ombi la mahakama lililotegemea habari za uongo, bila idhini sahihi,” Bw.Mutiso aliambia Taifa Leo.

“Hata hivyo, pia ilidhihirika kuwa wateja wangu walihojiwa katika mazingira ya kulazimishwa. Walisema walilazimishwa kutia saini taarifa, na maswali waliyoulizwa yalionyesha kuwa serikali ilikuwa ikijaribu kuwahusisha na makala ya BBC ya hivi majuzi,” aliongeza.

Haya yamejiri huku BBC ikisema Jumamosi kwamba vijana hao hawakuhusika kwa vyovyote kutayarisha makala hayo.

“Tumefahamishwa kuhusu kukamatwa kwa wanahabari wanne nchini Kenya. Ili kuwa wazi, hawakuhusika kwa njia yoyote kutayarisha makala ya BBC Africa Eye: Blood Parliament,” ilisema ofisi ya habari ya BBC katika taarifa.

Makala hayo yaliwataja maafisa kadhaa wa usalama wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja na mauaji ya waandamanaji wasiokuwa na silaha.

Wanne hao waliachiliwa Jumamosi, Mei 3, dakika chache baada ya saa nne asubuhi, kufuatia kilio cha umma kuhusu kukamatwa kwao.