Habari za Kitaifa

Wakili ‘The Grand Mullah’ akunja mkia, aomba Mahakama ya Juu imuondolee marufuku

Na JOSEPH WANGUI January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAJAJI wa Mahakama ya Juu wanatafakari kuhusu kesi mpya iliyowasilishwa kuirai ifute marufuku iliyomwekea Wakili mashuhuri Ahmednasir Abdullahi.

Mahakama hiyo ilimpiga Bw Abdullahi marufuku kuwakilisha mteja yeyote mbele yao na uamuzi ambao unatarajiwa huenda ukatuliza au kuzidisha taharuki kati yake na majaji hao.

Marufuku hiyo iliyotangazwa Januari 2024 baada ya Bw Abdullahi kukashifu vikali mahakama mitandaoni, ilisababisha mgogoro mkali uliofikia Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC) na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).

Kesi kadhaa ziliwasilishwa zikilenga kuwaondoa majaji wa Mahakama ya Juu, ikiwemo Jaji Mkuu Martha Koome, majaji hao wakishutumiwa kwa kusakama uhuru wa kuzungumza na kutumia vibaya mamlaka yao

Jana, Mawakili Paul Muite na Fred Ngatia walihimiza mahakama ya juu itafakari upya uamuzi wake wakihoji kuwa Bw Abdullahi amejisaili nafsi na kulalamika kwamba marufuku hiyo ya miaka miwili ishatimiza malengo yake.

Suala hilo lilizuka katika kikao cha kwanza cha korti mwaka huu mbele ya jopo la majaji sita wakiongozwa na Jaji Mkuu.

Kikao hicho kilianza na kimya cha dakika moja kwa heshima ya marehemu Jaji Mkuu Mohammed Ibrahim, aliyeaga dunia Disemba.

Korti kisha iligeukia mgogoro uliodumu miongo mingi kati ya serikali na kampuni ya ardhi ya Nguruman Limited.

Hata hivyo, kikao hicho kilichukua mkondo usiotarajiwa kufuatia ombi lililotolewa kwa mdomo na Mabw Muite, Ngatia, wakimwakilisha Bw Abdullahi, waliohimiza korti kutafakari upya uamuzi wake wa kumpiga marufuku wakili huyo.

Bw Abdullahi hapo mbeleni aliwakilisha kampuni ya Nguruman katika mahakama ya rufaa, ambapo shirika hilo lililipwa fidia ya Sh17 bilioni kuhusu kuingiliwa mara kwa mara na serikali kukosa kulinda mali yake.

Serikali ilikata rufaa katika Mahakama ya Juu ikilenga kuzima fidia hiyo.

Mawakili hao walihoji kwamba marufuku hiyo, iliyomzuia Bw Abdullahi na kampuni yake kufika mbele ya Korti ya Juu tangu Januari 2024, “imetimiza kusudi lake” na inapaswa kufutwa.

“Kumkataza kufika mbele ya majaji kumetimiza lengo lake, na tunaomba kwamba amri hiyo iondolewe,” alisema Bw Muite, akihoji kwamba wasilisho hilo lilifuatia mdahalo na wakili husika.

Bw Ngatia aliongeza kwamba miaka miwili imepita tangu kikwazo hicho kilipowekwa, kuruhusu muda wa kutosha kutafakari.

Hata hivyo, majaji walijibu kwa makini. Jaji Isaac Lenaola aliwashinikiza mawakili kutoa hakikisho thabiti kwamba Bw Abdullahi hatarejelea tabia yake.