Wakulima bado wanatatizika kupata mbolea nafuu uhaba ukishuhudiwa
WAKULIMA wanatatizika kupata mbolea ya ruzuku kutoka kwa Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) na maduka ya rejareja msimu wa mvua ya masika ukitarajiwa.
Wakulima hao hawana chaguo isipokuwa kusubiri shehena mpya kuwasilishwa na serikali au kununua pembejeo hiyo kwa bei ya juu.
“Tumepewa ahadi kwa zaidi ya wiki tatu kwamba mbolea hiyo italetwa na serikali, lakini hilo halijatokea na hatujui kama itawasili wakati wowote hivi karibuni,” alisema Bw David Rotich, mkulima kutoka Kaunti ya Bomet.
Sawa na mamia ya wakulima ambao wameandaa mashamba yao kwa upanzi, Bw Rotich anakabiliwa na hatari mbili — kusubiri mbolea ambayo haijulikani lini itawasili huku magugu yakikua shambani, jambo ambalo litamsababishia gharama ya ziada ya kulima tena, au kununua mbolea kutoka maduka ya rejareja kwa bei ghali.
Gunia la kilo 50 la mbolea ya ruzuku aina ya NPK linauzwa kati ya Sh 2, 500 na Sh 6, 500 katika maduka ya biashara kote nchini.
Rais William Ruto alianzisha mpango wa mbolea ya ruzuku mapema 2023, hatua iliyosababisha kupungua kwa bei na kuongezeka kwa uzalishaji kwani ilipunguzia wakulima gharama.
Bi Janeth Yegon, mkulima kutoka Elkerin, Kaunti ya Narok, alisema katika mahojiano na Taifa Leo kuwa serikali inapaswa kusajili wakulima upya ili kupata takwimu sahihi za wanaohitaji pembejeo za kilimo.
“Ni wazi kuwa idadi ya wakulima wanaojihusisha na kilimo sasa ni kubwa ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita. Serikali inapaswa kuweka sajili wazi ili kuongeza wakulima zaidi na ukubwa wa mashamba yao,” alisema Bi Yegon.
Bi Juliana Mengech, mkulima kutoka eneobunge la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru, alisema kuwa wakulima wengi katika eneo hilo hawajafikiwa na mpango wa serikali.
“Kwa nini serikali haiwezi kurekebisha orodha ya wanaonufaika kila mwaka, ilhali tunajua kwamba kutokana na mpango wa ruzuku, eneo la kilimo limeendelea kupanuka?” Bi Mengech alihoji.
Serikali imekuwa ikisambaza mbolea nchini kulingana na idadi ya wakulima waliosajiliwa na kiasi cha mbolea wanachohitaji.
Hata hivyo, kumekuwa na uhaba mkubwa wa mbolea nchini huku ripoti zikionyesha kuwa baadhi ya wakulima wameuziwa mbolea bandia na wafanyabiashara walaghai.
Katibu wa Kilimo, Dkt Paul Ronoh, alikiri kuna mahitaji ya juu ya mbolea yanayopita kiwango kilichopangwa na serikali na yamesababisha uhaba unaoshuhudiwa nchini.
Dkt Ronoh alisema kuwa ingawa serikali hivi karibuni ilisambaza magunia milioni 3.5 katika vituo vya NCPB, bado kuna upungufu wa zaidi ya magunia milioni moja ya mbolea nchini.
Dkt Ronoh alisema kuwa ingawa serikali hivi karibuni ilisambaza magunia milioni 3.5 katika vituo vya NCPB, bado kuna upungufu wa zaidi ya magunia milioni moja ya mbolea nchini.
Alisema mbolea ya ruzuku ilisafirishwa hadi vituo vya NCPB Jumatatu wiki hii (Machi 24, 2025), lakini imebainika kuwa maduka mengi bado hayajapokea pembejeo hiyo.
Dkt Ronoh aliwataka wakulima kuwa na subira.
Lakini wakulima katika eneo la South Rift wameitaka serikali kuhakikisha kuwa usambazaji wa mbolea haukatizwi kwani msimu wa upanzi umebadilika, huku wakulima wakijihusisha na kilimo mseto.