• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:28 PM
Wakulima walia mgao wa mbolea nafuu ukipunguzwa

Wakulima walia mgao wa mbolea nafuu ukipunguzwa

NA BARNABAS BII

WAKULIMA wamejipata pabaya baada ya serikali kupunguza mgao ambao uliwekewa mbolea ya bei nafuu kutoka Sh16.2 bilioni hadi Sh10 bilioni.

Hatua ya kupunguza mgao huo ipo katika makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa kifedha. Hazina Kuu ya Fedha inatarajiwa kuzindua bajeti ya Sh3.9 trilioni ya 2024/25 itakayopitishwa na Bunge mwezi Juni.

Inahofiwa kuwa wakulima wadogo huenda wakaathirika zaidi na hatua ya kupunguza bajeti katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.

Serikali ya Kenya Kwanza ilipanga kufanyia sekta hiyo mageuzi makubwa ili wakulima nao wanufaike na kupata faida.

Hata hivyo, wakulima sasa wanalalamikia kupunguzwa kwa mgao huo wa fedha ambazo zimetengewa ununuzi wa mbolea.

Wanasema hatua hiyo itarejesha nyuma hatua zilizopigwa kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula.

“Wakulima wamekuwa wakipoteza katika migao iliyopita kutokana na pesa kupunguzwa. Inasikitisha kuwa bei ya pembejeo zao ipo juu na soko halipo vizuri ilhali serikali inapunguza mgao,” akasema Bw Kipkorir Menjo, Mkurugenzi wa Chama cha Wakulima Nchini wakati wa mkutano na wakulima mjini Eldoret.

Makadirio ya bajeti ya 2024/25, yanaonyesha kuwa sekta ya kilimo itapokea Sh47.45 bilioni licha ya jukumu kubwa linalotekelezwa kuimarisha uchumi wa nchi.

Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u, anatarajiwa kuwasilisha bajeti hiyo wakati ambapo gharama ya maisha inaendelea kupanda na bei ya bidhaa za kimsingi zikiendelea kupanda pia.

Wakulima wengi katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, ambalo ni ghala la taifa, wanapanga kupunguza kiwango cha ardhi ambacho kipo chini ya kilimo cha mahindi. Wanalenga kuchukua hatua hiyo kwa sababu ya kupunguzwa kwa mbolea hiyo ya gharama ya chini.

“Kupunguzwa kwa mgao wa mbolea ya bei nafuu ina maana kuwa wakulima wengi watatuma maombi kupata pembejeo chache za kilimo,” akasema Mzee Pius Kirwa kutoka Ziwa, Uasin Gishu.

Alipendekeza kuwa serikali inastahili kutengea angalau asilimia 10 ya bajeti ya nchi kwa sekta ya kilimo.

Mbolea ya serikali ya bei nafuu, inauzwa kwa Sh2,500 kwa kila gunia la kilo 90 lakini mbolea hiyo imegubikwa na sakata.

Madukani, mbolea hiyo inauzwa kwa Sh5,400 gharama ambayo inawashinda wakulima wengi kuimudu.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi njama ya kuua Azimio ilivyotibuka

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Je, mafuriko haya yanatufunza nini...

T L