Habari za Kitaifa

Wakulima waliopoteza mazao kwa mafuriko kukosa fidia

May 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

PENDEKEZO la maseneta kwamba Serikali ya Kitaifa iwalipe fidia wakulima ambao mimea yao ya chakula iliharibiwa na mafuriko kulipwa fidia limegonga mwamba.

Hii ni baada Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kuliambia bunge la Seneti kwamba wizara yake haiwezi kutoa fedha za kuwalipa wakulima walioathiriwa bila kuwepo kwa mgao wa bajeti.

“Mpango wa serikali wa kushughulikia madhara yaliyosababishwa na mafuriko haujumuishi ulipaji ridhaa kwa wakulima na wafugaji walioathiriwa na mafuriko. Hatuna mgao wa bajeti uliotengwa kwa ajili ya kuwalipa ridhaa wakulima,” Bw Linturi akawaambia maseneta Jumatano.

Aidha, waziri alifichua kuwa serikali haijatathmini kiwango cha uharibifu wa mimea uliosababishwa na mafuriko kote nchini.

“Utathmini huo utaanza baada ya msimu wa mvua ya masika kumalizika,” Bw Linturi akasema.

Waziri huyo wa Kilimo alitoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali kutoka kwa Seneta wa Tana River Danson Mungatana.

Bw Mungatana alitaka kujua ikiwa serikali itawafidia wakulima wenye mashamba katika mipango ya unyunyiziaji ya Bura, Tana, Hola na maeneo mengine katika Kaunti ya Tana River ambayo yalifunikwa na maji ya mafuriko.

Mazao yanayokuzwa katika mashamba hayo ni kama vile maembe, ndizi, machungwa, mahindi, matikitimaji miongoni mwa mimea mingine. Takriban mashamba ya ukubwa wa ekari 10,000 yaliathirika na mafuriko.

“Mimea ya mazao iliyoharibiwa na mafuriko katika mashamba yote katika kaunti ya Tana River inakadiriwa kugharimu karibu Sh700 milioni. Aidha, kaunti yetu ilipoteza mbuzi 680, kondoo 510 huku sehemu kubwa ya kulishia mifugo ikiharibika,” Bw Mungatana akasema.

Waziri Linturi alisema kuwa Wizara yake iko chonjo kukabiliana na magonjwa ya mifugo yanayosambazwa na wadudu wanaoletwa na mvua.

“Wakati huo huo, tunaendelea kununua chanjo na dawa zingine za kuangamiza magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo kama vile ng’ombe, kondoo, mbuzi, ngamia miongoni mwa mifugo mingine. Kufikia sasa tumenunua dozi 1.4 milioni za chanjo ya ugonjwa wa Rift Valley Fever na dozi 450,000 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa blue tongue,” Bw Linturi akaeleza.