Habari za Kaunti

Wakulima wapata hasara ya mamilioni ndovu wakivamia mashamba yao

Na MWANGI NDIRANGU November 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA katika kaunti za Nyeri na Laikipia wamepata hasara ya mamilioni baada ya ndovu kuyavamia mashamba yao siku tatu mfululizo.

Wanyama hao wanaosemekana kutoka msitu wa Mlima Kenya kuelekea eneo la Laikipia wamesababisha uharibifu katika mashamba zaidi ya 20, na kuharibu mimea iliyokuwa karibu kuvunwa.

Mlinzi wa Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya anayesimamia eneo la Laikipia Mashariki, David Mwasi, alithibitisha kuwa kuna takriban makundi matano ya ndovu ambao wamekuwa wakitoka Msitu wa Mlima Kenya kuelekea Laikipia katika maeneo ya karibu na Hifadhi ya Ol Pejeta.

“Wanyama hao wanahama kutoka msituni hadi eneo laa Laikipia kufuatia mvua kubwa inayonyesha. Tunafanya doria za usiku ili kupunguza uharibifu kwenye mashamba,” akasema Bw Mwasi.

Mmoja wa wakulima ambao shamba lake lilivamiwa Bi Anne Wanjiru kutoka kijiji cha Ichuga Kaunti ya Nyeri, alisema amepata hasara ya zaidi ya Sh300,000 baada ya ndovu hao kuingia katika shamba lake la ekari mbili.

“Tembo hao wamekuwa wakitembelea shamba langu kila usiku tangu Jumanne jioni na wameharibu aina mbalimbali za mimea. Tumekuwa tukipigia mamlaka simu lakini wamekuwa wakija baada ya mimea yetu kuharibiwa,’ akasema Wanjiru.

Mkulima mwingine Bi Ann Muriuki alisema aliona kundi la zaidi ya ndovu 30 wakivamia shamba lake Jumatano usiku na hakuweza kufanya lolote.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO