• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Wakulima wauziwa manyoya ya mbuzi na changarawe kama mbolea ya kisasa

Wakulima wauziwa manyoya ya mbuzi na changarawe kama mbolea ya kisasa

NA CHARLES WASONGA

MAAFISA wa upelelezi katika Kaunti ndogo ya Koibatek iliyoko Kaunti ya Baringo wamearifiwa kuhusu sakata ambapo wakulima wanauziwa mchanganyiko wa punje za chumvi lishe ya ng’ombe, mawe meusi na manyoya ya mbuzi au kondoo eti ni mbolea ya kisasa ya NPK.

Maafisa hao wameanza uchunguzi kuhusu ulaghai huo baada ya kupashwa habari kwamba wakulima wawili waliuziwa magunia 34 ya mbolea hiyo feki kutoka ghala la Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) mjini Eldama Ravine.

Wakulima hao wanatokea kijiji cha Poror, kata ya Arama, katika Kaunti ndogo ya Koibatek.

Kulingana na ripoti ya polisi, wawili hao walinunua mbolea hiyo yenye lebo ya jina, KELGREEN, kwa Sh89,600.

“Baadhi ya sampuli zilizoletwa kwa afisi ya DCI mjini Eldama Ravine zilikuwa na punje zinazofanana na mchuvi ya ng’ombe na mawe mweusi na zingine zilikuwa na manyoya ya mbuzi au kondoo,” ikasema ripoti ya polisi iliyotolewa Jumamosi, Machi 23, 2024.

“Wakulima walipigwa na butwaa walipofungua magunia ya mbolea hiyo tayari kwa upanzi na kugundua kuwa haikuwa mbolea halisi,” ripoti hiyo ikongeza.

Kamati ya Usalama katika Kaunti Ndogo ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo, walikagua magunia ya mbolea yaliyonunuliwa na kuagiza meneja wa NCPB kuamuru magunia 2,650 ya mbolea hiyo, ambayo yalikuwa yamekwisha kuuziwa wakulima wengine, yarejeshwe.

Ufichuzi wa sakata hiyo unajiri siku chache baada ya mkurugenzi wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) Esther Ngari kuwaambia wabunge kwamba mbolea kwa jina ‘GPC Plus Organic Fertilizer’,  ambayo imekuwa ikiuziwa wakulima tangu mwaka 2023, ni feki.

Mbolea hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya SBL-Innovate Manufacturere Ltd, haikutimiza viwango vilivyowekwa kwa ubora wa mbolea asili.

Bi Ngari aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo kwamba kampuni hiyo ilipewa leseni ya kuuza mbolea asili chapa “BL-GPC Original” mnamo Januari 28, 2023 baada ya kutuma maombi Januari 13, 2023.

“Awali kampuni hii ilitimiza mahitaji yote ndipo Kebs ikaipa leseni ya kuuza mbolea asili. Lakini baadaye ilishiriki ulaghai kuwa kuuza mbolea feki kinyume cha sheria kuhusu viwango vya ubora,” akasema Alhamisi alipofika mbele ya kamati hiyo katika majengo ya bunge.

Alisema Kebs iliipa kampuni ya SBL-Innovate Manufacturer Ltd leseni ya kuuza mbolea asili lakini baadaye ikauza bidhaa hiyo feki iliyotengenezwa kwa “dolomite”, yenye madini ya ‘calcium’, ‘magnesium’, ‘carbonate’.

“Aina hii ya madini hutumika kuimarisha hali ya udongo wala sio kama mbolea ya kiasili,” Bi Ngari akaeleza.

Alisema Kebs alibaini ulaghai huo baada ya uchunguzi ambao maafisa wake waliendesha katika maduka ya bidhaa za kilimo mnamo Februari 2024.

“Baada ya sampuli 59 kupimwa, ilibainika kuwa hazikutimiza viwango vya mbolea asili,” Bi Ngari akasema.

Alisema operesheni iliyoendeshwa na maafisa wake ilisaidia kunaswa kwa magunia 5,840 ya kilo 25 ya mbolea hiyo feki.

“Hata hivyo, kufikia sasa hatujui kiwango cha mbolea hiyo ambacho kingali sokoni,” Bi Ngari akasema akijibu swali kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo John Mutunga.

KEBs ilisema kuwa imeanzisha mchakato wa kuishtaki SBL Innovate Manufacturers Ltd.

“Tumeandikia Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma achukue hatua za kisheria dhidi ya kampuni hiyo,” akasema Bi Ngari.

Wabunge walilivalia njuga suala hilo baada ya maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kunasa magunia kadhaa ya 700 ya mbolea inayodaiwa feki mjini Kakamega.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Mwadime aagiza baa zifunguliwe

Maafisa wanasa magunia 560 ya mbolea ‘feki’...

T L