Wakuu wa shule wakaidi wizara na kuongeza karo na ada nyinginezo
WAKUU wa shule nyingi kote nchini wamewataka wazazi kulipa karo ya ziada nje ya ile rasmi iliyowekwa na Wizara ya Elimu, wakitaja kutotengewa fedha za kutosha kuwawezesha kusimamia shule.
Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa, shule zimebuni mbinu mbalimbali za kutoza karo ya ziada na kuepuka kugunduliwa na wakaguzi wa hesabu au kuadhibiwa na serikali.
Baadhi wamerasimisha ongezeko la karo kwa kuwafanya wazazi kuidhinisha mabadiliko wakati wa mikutano mikuu ya kila mwaka.
Katika baadhi ya matukio, ada haramu huwekwa kwenye akaunti tofauti na zile rasmi ambazo Wizara huweka fedha za shule.Ada za ziada ambazo wazazi wanaombwa kulipa zinalenga kukidhi mambo kama vile ufundishaji wa ziada, zinazojulikana kama motisha, ununuzi wa mabasi ya shule, sare kwenye maduka yaliyochaguliwa au kufadhili ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali shuleni.
Kwa kuzingatia muundo wa ada za ziada ulioonekana na Taifa Leo na ushahidi kutoka kwa wazazi, ada zilizofichwa pia hazionyeshwi katika maelezo ya karo ya wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali za kaunti, hazina ya Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge, na mashirika mengine.Wafadhili hulipa tu kiasi rasmi.
“Ada hizi zilizofichwa ambazo haziorodheshwi zimekuwa changamoto kwetu. Kuongezwa kwa karo na pesa za shule kulipwa katika akaunti tofauti za karo za shule lakini hazionyeshwi katika maelezo ya karo. Ni jambo ambalo Waziri wa Elimu Julius Ogamba lazima alishughulikie,” akasema Mbunge wa Ndaragua George Gachagua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu Joe Nyutu alisema wazazi kote nchini wanalalamikia ongezeko la karo za shule.Alisema wazazi wanalazimika kulipa karo ya ziada ambayo ni kati ya Sh2,000 hadi Sh18,000 na kuitaka serikali kuwa makini. “Maelezo hayo ya karo ya ziada yanatumwa kupitia ujumbe mfupi wa simu ,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA