Habari za Kitaifa

Walimu njia panda vyama vikizozana na serikali kuhusu bima ya afya SHA

Na  MERCY SIMIYU September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WALIMU wanakabiliwa na sintofahamu huku vyama vya kutetea maslahi yao vikizozana na serikali kuhusu mpango wa kuwahamisha kutoka bima ya afya ya Minet ya thamani ya Sh20 bilioni hadi Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Viongozi wa vyama vya walimu wameonya kuwa mabadiliko haya yanayotarajiwa kuanza kufuatia kuisha kwa mkataba wa sasa na kampuni ya Minet mwezi ujao yanaweza kuleta mgogoro mkubwa.

Mkataba wa Minet unamalizika mwezi ujao, na viongozi wa vyama vya walimu wanahofia kuwa mpito wa ghafla unaweza kuwanyima walimu zaidi ya 400,000 matibabu, ingawa maafisa wa serikali wanasema SHA itawawezesha walimu kupata vituo vya afya zaidi vya afya kuwahudumia.

Ijumaa iliyopita, viongozi wa vyama vya walimu walikutana na Tume ya Huduma za Walimu (TSC), maafisa kutoka Ofisi ya Rais, na wawakilishi wa SHA. Katika kikao kilichofanyika katika afisi za TSC jijini Nairobi, SHA walieleza mpango wao wa kuwapatia walimu upatikanaji wa zaidi ya vituo 9,000 vya afya nchini, ikilinganishwa na vituo takriban 800 vinavyopatikana sasa chini ya Minet.

Walikubaliana kuwa mazungumzo zaidi yatafanyika kabla ya mabadiliko yoyote kufanyika.Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Kenya (Knut), Collins Oyuu, amesema hawataharakisha kuunga mkono pendekezo la serikali la kuhamisha bima ya afya kutoka Minet kwenda SHA.

Alisisitiza kuwa kwa kuwa walimu zaidi ya 400,000 wa shule za serikali na mamilioni ya wanaowategemea wataathirika, maamuzi kama haya yanahitaji ushauri wa kina kutoka kwa wanachama wa chama.“Mambo haya lazima tuyarudishe kwa wanachama wetu kwa uangalifu mkubwa.

SHA ilituonyesha mambo kadhaa jana, lakini kwa maoni yetu, mchakato bado haujakamilika. Tunaona ni sawa kupeleka suala hili kwa Baraza Kuu la Taifa (NEC) kwa uamuzi wa mwisho,” alisema.

Hitilafu kuu ni kwamba bima ya sasa ya Minet itamalizika mwezi ujao. Katibu Mkuu alizungumzia pia hotuba ya Rais William Ruto Ikulu, ambapo alitoa ahadi ya kuchunguza bima ya afya kwa walimu.

“Rais alisema atachunguza bima ya afya, watu walidhani tayari ni kuhusu SHA. Ndio, alishauriana na vyama vya walimu, lakini tunapaswa kuwa wazi: alisema atafanya mapitio ya bima ya afya, si kuwahamisha walimu wote kwa ghafla SHA. Mapitio ni mazuri, lakini kuhamisha walimu kwa SHA yote yanahitaji mashauriano ya kina,” alifafanua.

Viongozi wa Kuppet wamesema kuwa serikali ina nia ya kuhamisha walimu haraka bila ushauri wa kutosha, jambo litapata upinzani mkali.Kaimu Afisa Mkuu mtendaji wa TSC, Evaleen Mitei, ameambia Kamati ya Elimu ya Bunge kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu mpango huo wa kuhamisha walimu hadi SHA ifikapo Desemba 1.

Vyama vya walimu vinaonya kuwa walimu hawawezi kulazimishwa kujiunga na mpango usio na uwazi wala hakikisho kuhusu haki zao.Viongozi hao pia wamelalamikia huduma duni chini ya Minet ikiwemo ucheleweshaji wa ruhusa za matibabu na mizozo kati ya madaktari na kampuni ya bima, ambayo inadhaniwa kutilia mkazo faida zaidi kuliko huduma kwa walimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Afya na Ustawi wa Walimu Kenya, Ndung’u Wangenye, ameonya walimu wasihamishwe hadi wawe na bima inayojumuisha huduma zote muhimu za matibabu.Amesisitiza kuwa serikali inapaswa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha walimu na familia zao hawapati hasara chini ya mfumo mpya wa afya.

“Tutachunguza kila kitu kinachotolewa na SHA kwa sababu mwishowe, walimu walikuwa wakiteseka chini ya Minet. Bima hii mpya lazima iwe kamili kabisa, na ikiwa haitakidhi mahitaji ya walimu, hatutaweza kuikubali,” alisema.