Waliokamatwa kuhusu mauaji ya Mbobu waachiliwa huru; kikosi kipya cha wapelelezi chaundwa
KIKOSI kipya cha wachunguzi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Mauaji cha Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kimekabidhiwa rasmi uchunguzi wa mauaji ya wakili Mathew Kyalo Mbobu.
Watu watatu waliokuwa wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo waliachiliwa Jumamosi usiku baada ya uchunguzi kuonyesha hawakuhusika.
Wachunguzi wapya walipitia taarifa zilizorekodiwa na maafisa wa DCI wa Lang’ata na kuamua kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuwazuilia wanaume hao waliokuwa mahabusu tangu Alhamisi usiku.
Waliokuwa wamekamatwa ni Bw George Wainaina, afisa wa chama cha KANU; Bw Paul Mbugua ambaye ni jamaa wa Wainaina; na Bw Eric Gichuhi, rafiki wa marehemu Mbobu.
Walikamatwa na maafisa wa Kikosi cha Operesheni Maalum (OSU) baada ya video ya CCTV kuonyesha walikuwa kati ya watu wa mwisho kuonana na wakili huyo.
Wainaina aliwaambia polisi kuwa alikutana na Mbobu na Gichuhi katika hoteli ya Sargret, Nairobi.
Alieleza kuwa alifika huko kukutana na mfanyakazi wake ili kumpa hundi. Mbobu na Gichuhi walikuwa wakiondoka na walibadilishana salamu tu kabla ya kuagana.
Gichuhi, ambaye aliwahi kusoma na Mbobu katika Chuo Kikuu cha Nairobi na huishi naye Karen, alisema walikutana kwa chakula cha mchana, kisha Mbobu akarudi ofisini.
Kwa upande wake, Mbugua alisema hamfahamu Mbobu, na alikuwa hotelini kukutana na bosi wake.
Wainaina aliambia Taifa Leo kuwa alishtuka kukamatwa na akaeleza kuwa polisi walimvamia nyumbani na kuchukua Sh50 milioni.
“Nilikamatwa ghafla bila hata kupewa muda wa kubadilisha nguo. Nilitupwa kwenye seli baridi katika kituo cha polisi cha Kileleshwa,” alisema Wainaina.
Wainaina alisema maafisa wa DCI walimhoji kuhusu biashara aliyokuwa akifanya na wakili Mbobu, jambo ambalo alikanusha kabisa.
Wakili wake, Musa Maulid, alisema kukamatwa kwao hakukuwa na msingi wa kisheria, na ni matumizi mabaya ya mamlaka ya polisi.
“Tuna ushahidi wa uchunguzi wa simu, ukaguzi wa silaha na maelezo yaliyothibitishwa kuwa hawa watu watatu hawahusiani kwa vyovyote na mauaji haya,” alisema Maulid.
Alishangaa ni kwa nini polisi waliwalenga watu hao watatu pekee kati ya wengi waliokuwa kwenye hoteli.
Kwa sasa, wachunguzi wa mauaji wameelekeza juhudi zao kwenye kesi na mikataba ambayo marehemu Mbobu alikuwa akiendesha.
Mbobu aliuawa kwa kupigwa risasi Jumanne iliyopita na watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki akiwa Barabara ya Magadi.