Waliokosa kuripoti Gredi 10 kusakwa ili kusaidiwa, serikali yatangaza
WANAFUNZI kati ya 300,000 hadi 500,000 wa Gredi 10 bado hawajaripoti shule za Sekondari Pevu, huku Wizara ya Elimu ikianza ukaguzi maalum ili kuwabaini wale ambao hawajaanza masomo.
Kulingana na wizara hiyo, maafisa wa kila eneo wakiwemo machifu watatembelea familia ili kubaini sababu zinazowafanya baadhi ya watoto kutojiunga na shule na kutafuta njia bora za kuwasaidia.
“Mchakato wa mpito hadi sekondari pevu utatekelezwa kikamilifu huku wizara ikilenga kufikia asilimia 100. Wiki ijayo, maafisa watashirikiana na Waziri wa Usalama wa Ndani ili machifu na wasimamizi wa maeneo watembelee nyumba za wanafunzi kubaini sababu za kutoripoti shuleni na kubuni mbinu za kuwasaidia,” alisema Waziri wa Elimu katika mahojiano na Taifa Jumapili.
Wizara ya Elimu imefafanua kuwa takwimu za sasa zinazoonekana kwenye mfumo wa mtandaoni wa usajili wa shule za sekondari hazionyeshi idadi kamili ya wanafunzi waliosajiliwa, kwa kuwa shule bado zinaendelea kupakia rekodi kutoka kwa usajili wa ana kwa ana.
Akizungumza na Taifa Jumapili Waziri Ogamba alisema kuwa ingawa mfumo wa mtandaoni unaonyesha baadhi ya shule zikiwa na idadi ndogo ya wanafunzi, kwa hali halisi idadi ya wanafunzi wanaohudhuria masomo ni kubwa zaidi.
“Wanafunzi bado wanaendelea kuripoti. Kufikia jana usiku, wanafunzi 550,000 tayari walikuwa wameingizwa kwenye mfumo, na tulikuwa tunasubiri maeneo mawili yaingize takwimu zao. Usajili wa ana kwa ana uko juu zaidi kuliko takwimu zinazoonekana kwenye mfumo,” alisema Bw Ogamba.
Aliongeza kuwa katika visa vingi, wanafunzi tayari wamepokelewa shuleni, wamepata mafunzo ya utangulizi na kuanza masomo, lakini taarifa zao bado hazijaingizwa kikamilifu kwenye mfumo kutokana na changamoto za mtandao katika baadhi ya shule.
Wizara pia ilieleza changamoto ya shule zisizo na wanafunzi wengi, ikisema kuwa baadhi ya taasisi zina idadi ndogo ya wanafunzi kutokana na ukosefu wa mahitaji.
“Lazima tukubali uhalisia—baadhi ya shule hazipendwi na wanafunzi. Hili litasaidia kufanya maamuzi ya baadaye kuhusu kuunganisha rasilmali katika shule zinazohitajika zaidi. Ripoti itaandaliwa baada ya zoezi hili kukamilika, ikionyesha idadi ya wanafunzi waliopokelewa na kila shule na iwapo kutahitajika marekebisho, ikiwemo kuwahamisha wanafunzi,” alisema.
Waziri wa Elimu pia alitangaza kuwa wizara imeongeza muda wa usajili wa wanafunzi wanaojiunga na Gredi 10 hadi Jumatano ijayo, kwa lengo la kufikia mpito wa asilimia 100 na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma, huku tathmini ikiendelea na baadhi ya maeneo yakichelewa kupakia ripoti.
Alisema uamuzi huo ulitokana na kuchelewa kwa ukusanyaji wa takwimu kamili za kuripoti, hasa katika maeneo ya Mashariki na Kaskazini Mashariki ambayo bado hayajawasilisha idadi zao za mwisho.
“Tumelazimika kuongeza muda wa mwisho wa usajili wa wanafunzi wa Gredi 10 hadi Jumatano ijayo ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nje, isipokuwa katika visa maalum vinavyohusisha makosa ya wazi ya uteuzi wa shule,” alisema Bw Ogamba.
Jumla ya watahiniwa milioni 1.3 walifanya mtihani Sekondari Msingi Kenya (KJSEA) mwaka 2025, ambao matokeo yake yalitolewa Desemba 2025.