Walitaka kuniua kwenye shambulio Limuru, asema Gachagua
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amezungumza baada ya mashambulizi dhidi yake wakati wa mazishi mjini Limuru siku, Alhamisi.
Katika taarifa ndefu, alifichua kuwa wahuni hao walimfuata akielekea kwenye gari lake na kulirushia kwa na kulipiga kwa vyuma.
“Leo, nilikuwa kwenye ibada ya mazishi huko Limuru ya kijana anayeitwa Erastus Nduati. Tulipokuwa tukijiandaa kumzika kijana huyo, majambazi walitushambulia sisi na waombolezaji wengine waliokuwepo, wakiwemo watoto,” Gachagua alisema.;
Akasema: “Kama Wakenya wanavyofahamu vyema mapema wiki hii serikali iliondoa maafisa wa usalama wa mwisho waliokuwa wakinilinda baada ya mchakato wa kuniondoa mamlakani tunaopinga.
Hata hivyo hatukuzungumzia uamuzi huu wa serikali ingawa matarajio ni kwamba Mkenya yeyote ambaye amehudumu katika ngazi ya serikali ambayo nilibahatika kuhudumu, analindwa na serikali hata baada ya kuondoka afisini.
Hata hivyo, sasa inaonekana kama uamuzi wa kuondoa usalama wangu ulikuwa wa kuniacha katik hatari ya aina ya mashambulizi ambayo tumeshuhudia leo.
Leo, nilikuwa kwenye ibada ya mazishi huko Limuru ya kijana anayeitwa Erastus Nduati. Tulipokuwa tukijiandaa kumlaza, wakora walituvamia na waombolezaji wengine wakiwemo watoto. Majambazi hao walikuwa wamejihami kwa mawe, mapanga, vyuma na fimbo.
Walituvamia waombolezaji waliokuwepo na kuwashambulia kwa kutumia silaha walizokuwa nazo. Kundi moja lilinifuata nilipokuwa nikienda kwenye gari langu, ambalo walianza kulishambulia kwa mawe na vyuma. Tuliondoka tukirushiwa mvua ya mawe!
Hii ni hali ya kusikitisha sana na aibu sana kwa serikali, ambayo ilikuwa wazi ilishiriki katika vitendo hivi. Tunakumbuka hasa familia iliyokuwa na mpendwa kwenye jeneza, ambayo ililazimika kukimbilia usalama licha ya huzuni yao kuu.
Hatutaogopa kusimama na Wakenya wanaohitaji tuwaunge mkono katika nyakati zao za shida. Tunatarajia tukio kama hili la aibu halitajirudia.
Majambazi hao walivamia hema lililotengewa viongozi wakuu kabla ya Gachagua kuitwa kutoa hotuba yake na kusababisha umati kutoroka ili kujilinda.
Kulingana na ripoti, watu kadhaa pia walipata majeraha mabaya huku picha za tukio hilo zikionyesha viti vya plastiki vilivyotawanyika kote.
Baada ya shambulio hilo, mshirika wa karibu wa Gachagua na seneta wa Kiambu Karung’o Thangwa aliwahakikishia umma naibu rais huyo wa zamani alikuwa salama.
Thang’wa, katika taarifa iliyotolewa saa chache baada ya tukio hilo, aliondoa hofu kwamba Gachagua alipata majeraha kufuatia tukio hilo.
‘’ Lilikuwa ni jaribio la mauaji. Lakini Naibu Rais wa wananchi yuko salama. Asanteni sana watu wa Limuru kwa kutuhakikishia usalama. Hatutatishika wala kunyamazishwa—sasa tunajua!’’ Thang’wa alisema.
Shambulio hilo linafuatia mzozo wake mkali na Rais Ruto.
Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa la AIPCA, Gachagua alimlaumu kiongozi wa nchi kwa kukosa kutii ushauri wake kuhusu mikataba ya Adani. Kulingana na Gachagua, licha ya kumuonya Ruto kuhusu mpango huo, rais alikosa kusikiliza ushauri wake.
“Nilimwambia rais mpango huu wa Adani ulikuwa na dosari na wananchi hawakuutaka, akanidharau kwa hilo. Na alisema wazi nilikuwa nikipinga miradi ya serikali,” Gachagua alisema.