• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Wamalwa akataaa marupurupu ya Nadco

Wamalwa akataaa marupurupu ya Nadco

NA MOES NYAMORI

KIONGOZI wa DAP Kenya, Eugene Wamalwa amekataa kupokea marupurupu ya kushiriki vikao vya Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano (NADCO) ambayo yanakadiriwa kuwa zaidi ya Sh1milioni.

Bw Wamalwa ambaye alikataa kutia saini ripoti ya mwisho ya Nadco kwa msingi kuwa haikutatua kupanda kwa gharama ya maisha, mnamo Ijumaa, Machi 8, 2024 aliandikia Makarani wa Seneti na Bunge la Kitaifa akikataa kulipwa pesa hizo.

Mnamo Ijumaa Bw Wamalwa pia hakuwepo wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo kwa Kinara wa Azimio Raila Odinga kwenye afisi zake za Capitol Hill, Nairobi.

Pia hakuwepo kwenye Ikulu wakati ambapo wanakamati waliwasilisha ripoti hiyo kwa Rais William Ruto.

Aidha, wanachama 10, wanane wa kiufundi na wanachama 20 wa sekreteriati mnamo Alhamisi walipokea barua kutoka kwa Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC) ikiwataka wawasilishe akaunti zao za benki.

“Nilikataa hadharani ripoti ya Nadco na kusema sitapokea marupurupu hasa kutokana na kutoshughulikiwa kwa gharama ya maisha. Naomba pesa ambazo nilifaa kulipwa zirejeshwe kwa Hazina Kuu ya Fedha,” akasema Bw Wamalwa kwenye barua iliyoandikwa Machi 8, 2024.

Karani wa Seneti, Bw Jeremiah Nyegenye Jumapili, Machi 10, 2024 alikataa kufichua kiwango cha marurupu ambayo wanakamati wa Nadco walistahili kulipwa.

Mnamo Septemba, Taifa Leo iliripoti jinsi ambavyo kamati hiyo ilitaka itengewe jumla ya Sh106 milioni kwa kipindi kizima mazungumzo yalipokuwa yakiendelea.

 

  • Tags

You can share this post!

Ujenzi wa bwawa na visima kupunguza mizozo

Ndondi: Friza apoteza kushiriki Olimpiki, Kenya Ikirudi...

T L