Habari za Kitaifa

Wamalwa: Ruto alikerwa nilipopeleka Wetangula, Musalia kwa Kenyatta

January 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MOSES NYAMORI

ALIYEKUWA Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa amefichua kuwa hatua yake ya kuwapeleka viongozi wa kisiasa wa upinzani kutoka magharibi mwa Kenya Moses Wetang’ula na Musalia Mudavadi kukutana na Uhuru Kenyatta katika Ikulu 2018, ndio chimbuko la uhasama wa kisiasa kati yake na Rais William Ruto.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Bw Wamalwa alisema Dkt Ruto alikerwa kiasi cha kumkabili na kumtaka aandike barua ya kujiuzulu kama waziri.

“Sababu ni kwamba nilipeleka Moses Wetang’ula na Musalia Mudavadi Ikulu kumwona Uhuru Kenyatta (Rais mstaafu) na kwamba tulikuwa tumeanzisha suala la umoja wa jamii ya Waluhya. Alihisi tungemzima kupenya eneo la Magharibi ilhali alipania kuwania urais 2022,” akasema.

“Kwanza tulikuwa na makabiliano makali na akauliza, unadhani wewe ni nani? Hii ni serikali yangu na Uhuru na ikiwa utawaleta hawa watu wa upinzani na ajenda yake ya umoja wa Waluhya, bure kabisa ondoka. Nataka barua yako ya kujiuzulu kesho,” Bw Wamalwa akaelezea jinsi Dkt Ruto alimfokea.

Hata hivyo, akasema, alipomwambia Bw Kenyatta kuhusu kisa hicho, alimshauri kupuuzilia mbali vitisho hivyo kwani yeye (Kenyatta) ndiye alimteua Waziri wa Ulinzi.

Bw Wamalwa alielezea kuwa kwa Dkt Ruto hatua ya kuwaleta Mbw Wetang’ula na Mudavadi kwa Bw Kenyatta baada ya handisheki ya Machi 9, 2018 kati ya Rais huyo mstaafu na Bw Raila Odinga ilikuwa njama ya kumtenga (Ruto) zaidi.

“Hata hivyo, baada ya mpango wa marekebisho ya katiba BBI kutibuka hatimaye Ruto alifaulu kuvutia Wetang’ula na Mudavadi upande wake na wakaanzisha muungano wa Kenya Kwanza. Alitamani sana kubuni muungano huo na bila shaka hatua hiyo ilichangia pakubwa ushindi wake,” Bw Wamalwa akaeleza.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa chama cha Democratic Action Party Kenya (DAP-K), alifafanua kuwa hana uhasama wowote wa kibinafsi na Rais Ruto bali ni mshindani wake kisiasa.

“Kumbuka tulibuni Jubilee pamoja na Dkt Ruto na Bw Kenyatta. Tukaunda serikali kwa misingi ya kuleta mwamko mpya wa uongozi wa kizazi kipya. Tulipokosana nilisalia na Uhuru Kenyatta. Na mimi na Dkt Ruto tukasalia marafiki, na simchukii kama adui. Namchukia kama mshindani wa kisiasa na ninaamini amepata marafiki wapya kutoka magharibi, Musalia na Wetang’ula. Nami nilipata marafiki wapya kama Raila na wengine,” anaeleza Bw Wamalwa ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Saboti.

Mwanasiasa huyo pia alitangaza azma yake ya kuwania urais 2027 akiungana na mwenzake katika Azimio Kalonzo Musyoka ambaye tayari ametangaza nia hiyo.

Bw Wamalwa alielezea kuwa kati ya viongozi wa upinzani wanaomezea mate kiti cha urais, yeye ndiye mwenye umri wa chini zaidi na mwenye maono mapya kwa taifa hili.

Hata hivyo, alikariri kuwa muungano wa Azimio umeungana licha ya vinara kadha kutangaza nia ya kuwania urais.

“Tutaweza kukubaliana kumwasilisha mgombeaji mmoja wa urais ambaye atafaulu kumwangusha Rais Ruto katika kinyang’anyiro cha 2027,” Bw Wamalwa akaeleza.