‘Wan Tam’ yatimia Malawi, Chakwera akiinua mikono baada ya kubwagwa na Mutharika
RAIS wa Malawi, Lazarus Chakwera, amekubali kushindwa katika uchaguzi wa urais uliofanyika Septemba 16, ambapo mgombeaji wa upinzani na rais wa zamani Peter Mutharika anaongoza kwa kura zaidi ya milioni moja.
Katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni chini ya saa mbili kabla ya Tume ya Uchaguzi ya Malawi kutangaza matokeo rasmi, Chakwera aliwashukuru Wamalawi wote kwa kumuunga mkono katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Bw Chakwera, alimpongeza Peter Mutharika, kwa kushinda katika uchaguzi huo.
Katika hotuba yake kwa taifa, Chakwera aliwashukuru Wamalawi kwa kumwamini kuiongoza nchi, akisema ataendelea kuwashukuru milele kwa imani na sapoti yao.
“Kwa sababu hii, dakika chache zilizopita nilimpigia simu Profesa Mutharika moja kwa moja kumpongeza kwa ushindi wake wa kihistoria na kumtakia mema katika kipindi chake kijacho kama Rais wa 7 wa Jamhuri ya Malawi.”
Matokeo ya awali yalionyesha Mutharika alipata takriban asilimia 66 ya kura halali katika majimbo 24 kati ya 36, huku Chakwera akipata asilimia 24 pekee.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, mgombeaji anatakiwa kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura halali ili ashinde moja kwa moja; vinginevyo, kunafanyika duru ya pili ya uchaguzi.
Wataalamu wa siasa walitabiri ushindani mkali kati ya Mutharika, mwenye umri wa miaka 85 na aliyekuwa madarakani kati ya 2014 na 2020, dhidi ya Chakwera, mwenye umri wa miaka 70.
Raia wa Malawi wamekumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi chini ya uongozi wa Chakwera, huku Mutharika akitambuliwa kwa kuboresha miundombinu na kupunguza mfumuko wa bei wakati wa utawala wake, ingawa amekuwa akikabiliwa na lawama za ubinafsi.
Tume ya Uchaguzi ya Malawi iliahidi kutangaza matokeo kamili ifikapo Septemba 24 baada ya kuchunguza kwa makini kila fomu ya matokeo, hasa baada ya Mahakama ya Katiba kukataa ushindi wa Mutharika mwaka 2019 kwa sababu ya kasoro katika uchaguzi, na kuagiza uchaguzi mpya mwaka 2020.
Malawi ni nchi ya Afrika Kusini-Mashariki yenye historia ndefu ya siasa za vyama vingi. Tangu kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1964, Malawi imepitia mabadiliko makubwa ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuhamia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1994.
Mwaka 2019, Malawi ilipata umakini mkubwa duniani baada ya uchaguzi wa rais kuhusishwa na dosari nyingi za kisheria na udanganyifu, ikiwemo matumizi ya rangi ya kurekebisha matokeo kwenye fomu za kura.
Hali hii ilisababisha Mahakama ya Katiba kufuta matokeo ya uchaguzi huo na kuamuru uchaguzi mpya kufanyika mwaka 2020, ambapo Lazarus Chakwera alichaguliwa kuwa rais.
Chakwera, ambaye ni mchungaji wa kanisa na kiongozi wa chama cha Malawi Congress Party (MCP), aliahidi kupambana na ufisadi na kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Hata hivyo, changamoto kubwa za kiuchumi, mfumuko wa bei na usimamizi mbaya wa rasilmali za umma zimekuwa kikwazo kikubwa kwa serikali yake.
Mutharika anajulikana kwa kufanikisha miradi ya miundombinu na kudhibiti mfumuko wa bei, ingawa amekuwa akikosoa kwa udhibiti duni na ubinafsi.