Wanachuo walia mgomo wa wahadhiri unawaharibia maisha
VIONGOZI wa wanafunzi wa baadhi ya vyuo vikuu nchini wamekerwa na mgomo wa wahadhiri ambao unaingia juma la tatu.
Hii ni baada ya juhudi za serikali kutatua matatizo ya wahadhiri kugonga mwamba wiki iliyopita.
Wanafunzi hao wanateta kuwa mgomo huo utaathiri mitihani ya mwisho wa muhula inayotarajiwa kufanywa Disemba.
Wakizungumza na wanahabari katika Chuo Kikuu cha Nairobi Jumapili, viongozi hao waliomba serikali ifanye hima kutekeleza matakwa ya wahadhiri yanayojumuisha nyongeza ya mishahara na marupurupu.
“Tunaomba serikali itafute suluhu ya kudumu na kusitisha mgomo ili kuhakikisha wanafunzi wanaokoa muda ambao umepotea na kuanza kurejelea masomo,” akasema Katibu Mkuu wa Muungano wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Zadock Okoth Nyakwaga.
Mfumo tata wa ufadhili wa elimu ya vyuo umetajwa kuwa miongoni mwa masuala yanayoathiri wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma.
Wanafunzi waliowekwa katika makundi ya ufadhili yasiyowafaa wanahangaika muhula huu wakiendelea kusihi serikali irekebishe makosa hayo.
Viongozi wa wanafunzi wamekashifu serikali kwa kuendelea kutetea mfumo ambao unapingwa vikali na wanafunzi, wazazi na mashirika ya kijamii.
Mnamo Oktoba 3, 2024, Jaji Chacha Mwita alitoa uamuzi wa kusitisha utekelezaji wa mfumo huo baada ya kesi kuwasilishwa na Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC).
“Tunaomba idara ya mahakama ifanye suala hili kuwa kipaumbele. Hatutarajii kingine ila uamuzi ambao utatupilia mbali mfumo mpya wa ufadhili wa elimu vyuoni,” alisema Bw Nyakwaga.
Kauli yake ilikaririwa na Kiongozi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chuka Adrian Oluoch ambaye alidokeza kuwa mgomo wa wahadhiri hauwaathiri wanafunzi tu, bali pia wazazi.
“Wanafunzi wamekuwa na muda mwingi sana wa kukaa bure na hakuna masomo yanaendelea vyuoni. Inavunja moyo kuona wanafunzi wakitoka chuoni Ijumaa na kurudi Jumatano kwa sababu hakuna mihadhara katika vyuo,” alisema Bw Oluoch.
Bw Masten Onyango, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, anasema kuwa hawajakamilisha hata nusu ya shughuli ya muhula huku wakitarajiwa kufanya mitihani.
Vile vile, wengine walifichua kuwa baadhi ya wahadhiri wanaendelea kufunza kupitia mitandao.
“Tuko chuoni lakini hatujui la kufanya. Ratiba ya mitihani imetolewa ilhali kozi nyingi hazijakamilishwa huku mijarabu mingi ikiwa haijafanyika,” Bw Onyango alisema.