• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:50 AM
Wanafunzi 12 Eldoret washtakiwa kwa kubugia pombe haramu

Wanafunzi 12 Eldoret washtakiwa kwa kubugia pombe haramu

NA TITUS OMINDE

SERIKALI mnamo Jumanne imebatilisha leseni zote za viwanda vinavyotengeneza pombe ya bei nafuu, hadi vitakapokaguliwa upya.

Hatua ya serikali inajiri huku tatizo la ulevi likiendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi ya nchi.

Bodi ya kutoa leseni na kukabiliana na pombe haramu katika Kaunti ya Uasin Gishu imeimarisha vita dhidi ya pombe haramu, ikifichua kuwa wanafunzi katika taasisi mbalimbali mjini Eldoret wamepotelea kwa pombe. Mbali na wanafunzi kubugia pombe haramu, mkurugenzi wa bodi hiyo Koiya Arap Maiyo alisema wananunua pia pombe inayouzwa kwa bei ya rejareja.

Alisema wanafunzi hao huendea pombe ambayo hupatikana kwa bei rahisi huku wangine wakinunua pombe kwa vipimo vya chini kinyume na sheria ambapo kuna aina ya pombe ambayo haistahili kuuzwa kwa viwango vya chini.

Pombe hiyo ya vipimo vya chini inauzwa kwa Sh20 hivyo kupewa jina ‘mbaombao’.

“Ni hatia kwa wauzaji wa pombe kuuza pombe kwa kutumia vipimo vya chini kinyume na viwango vinavyohitajika kisheria,” alisema Bw Maiyo.

Bw Maiyo alisema maafisa wa bodi hiyo wataendela na msako ili kulinda Wakenya dhidi ya pombe haramu.

Huku hayo yakijiri, wanafunzi 12 kutoka taasisi mbalimbali zilizoko mjini Eldoret walikamatwa wakiwa wamelewa na wakashtakiwa kwa kurusha matusi na kusababisha usumbufu katika maeneo ya umma.

Wakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Peter Ireri, walikubali mashtaka dhidi yao na kutozwa faini ya Sh2,000 kila mmoja au kuhudumia kifungo cha jela mwezi mmoja.

Takwimu kutoka bodi hiyo zimebaini kuwa mwezi mmoja uliopita, pombe aina ya chang’aa kiasi cha zaidi ya lita 5,000 ilinaswa mjini Eldoret.

Takwimu hizo zimebaini kuwa maeneo maarufu kwa biashara ya chang’aa ni mitaa ya Huruma, Langas, Munyaka, Kamukunji, Kahoya, na King’ong’o miongoni mwa maeneo mengine maarufu kwa biashara hiyo haramu.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa 21 wa uvamizi wa shamba la kibinafsi kuzuiliwa...

Mchekeshaji Dkt Cassypool adai ni chawa wa Rais

T L