Wanafunzi 2000 kunufaika na maktaba ya dijitali
Angalau wanafunzi 2,000 kutoka Gataka, Kaunti Ndogo ya Kajiado Kaskazini, watafaidika na maktaba ya kidijitali iliyoundwa kupunguza pengo la kiteknolojia.
Mradi huu wa thamani ya Sh 4 milioni umeanzishwa katika jengo la shule ya Nkaimurunya kwa msaada wa Women in Technology & Innovation Africa (WITIA), kwa ushirikiano na Rotary Club ya Karen.
Mradi huu wa mapinduzi unaleta teknolojia ya kisasa ya kujifunza katika moja ya shule za umma zenye upungufu mkubwa wa rasilmali katika maeneo ya miji midogo.
Maktaba ya Kidijitali ni mpango wa majaribio chini ya mpango mkuu wa WITIA, “Smart Libraries for a Smart Nation,” unaolenga kuwawezesha wanafunzi kupitia upatikanaji wa kidijitali, ubunifu, na elimu jumuishi.
Ikiwa na kompyuta 64 za kisasa, intaneti, na majukwaa ya masomo mtandaoni, Maktaba ya Kidijitali inawawezesha walimu na wanafunzi kupata nyenzo za elimu za kimataifa, kukuza utafiti, ubunifu, na ujuzi wa teknolojia.
Wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo ya kidijitali siku ya Ijumaa, wengi wa wanafunzi walisema kuwa hawajawahi kutumia kompyuta, wakitaja msaada huo kama “baraka kutoka kwa Mungu.”
Fantasia Baraka, 13, mwanafunzi wa Gredi 8, alisema kuwa nafasi ya kutumia kompyuta ilikuwa ndoto tu. Yeye anatoka familia ya kipato kidogo katika eneo hilo.
“Sijawahi kutumia kompyuta hapo awali. Hii ni nafasi adhimu ninayotarajia kuitumia kikamilifu. Nataka kuwa daktari wa watoto na najua teknolojia ya IT ni kipengele muhimu kufanikisha ndoto yangu,” alisema Baraka.
Wakati wa uzinduzi huo, maktaba ya kidijitali iliwawezesha wanafunzi kuanza mafunzo ya ujuzi wa kidijitali chini ya usimamizi wa walimu wao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nkaimurunya Comprehensive, Bi Charity Marinda, alisema kuwa ujuzi wa kidijitali kwa wanafunzi wasio na huduma za kutosha utawaweka sawa na wenzao waliyo na fursa nyingi.
“Shule yetu inahudumia jamii yenye upungufu mkubwa wa huduma, na Maktaba hii ya Kidijitali itabadilisha kabisa uzoefu wa wanafunzi wetu,” alisema Bi Marinda.
Mwanzilishi wa WITIA, Bi Eunice Pohlmann, alisema kuwa mradi huu hauhusiani tu na teknolojia bali unalenga kuunda fursa kwa watoto ambao vinginevyo wangebaki nyuma.
“Maktaba ya Kidijitali ni zaidi ya chumba chenye kompyuta — ni mlango wa fursa sawa. Kila mtoto, bila kujali hali yake, anastahili zana za kidijitali zinazounda mustakabali. Mradi huu wa majaribio utaenezwa hadi shule zingine zisizo na huduma za kutosha nchini Kenya,” alisema Bi Pohlmann.
Rais wa Rotary Club ya Karen, Bi Linet Ayuko, alisema kuwa ushirikiano huu utasaidia wanafunzi kuelewa nafasi za kidijitali kama fursa za kazi na maisha, huku akiongeza kuwa mradi utakuwa salama chini ya makubaliano ya pamoja (MOU) kati ya wadau na usimamizi wa shule.
“Maktaba ya Kidijitali inaonyesha jinsi ubunifu na ushirikiano vinavyoweza kubadilisha jamii na kufungua fursa mpya kwa wanafunzi,” alisisitiza Bi Ayuko.
Maktaba ya Kidijitali ya Nkaimurunya inasimama kama mfano wa majaribio wa kijamii, ikionyesha jinsi ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi unaweza kuharakisha maendeleo ya Kenya kuelekea Ajenda ya Taifa 2030 na Malengo ya Maendeleo Endelevu.