Habari za KitaifaMakala

Mkasa wa Endarasha: Wanafunzi jasiri walivyowakoa wenzao

Na STEPHEN MUNYIRI September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NI kitendo ambacho yamkini watu wengi wazima wangekiepuka, lakini Louis Karinga, mwenye umri wa miaka 12, kwa ujasiri na kujitolea, aliingia katika bweni lililokuwa likiteketea katika shule ya Hillside Endarasha, Kaunti ya Nyeri ili kuwanusuru wenzake wawili.

Kijana huyo shujaa alifanikiwa kutoroka bila majeraha kwenye bweni lililokuwa likichomeka baada ya kuruka kupitia dirisha lakini alipogundua kuwa rafiki zake wawili wa karibu walikuwa bado wamenaswa mle ndani, aliamua kurudi jengoni na kufanikiwa kuwavuta hadi mahali salama.

Hata hivyo, katika harakati za uokoaji alivuta moshi mwingi na kuishia hospitalini. Akisimulia masaibu yake katika Hospitali ya Mt Kenya mjini Nyeri, Karinga, ambaye alikuwa na babake Paul Ngumo, alikumbuka matukio ya usiku wa maafa.

Karinga alikuwa amelala kwenye bweni alipozinduliwa usingizini na ‘joto jingi’.

Alipoamka, bweni lilikuwa limewaka moto, moshi ukifuka katika kona zote.

Karinga alisema kitanda chake kilikuwa karibu na dirisha na alipogundua hatari iliyomkabili, alifanikiwa kumwamsha mwenzake aliyekuwa bado amelala na wote wawili wakaruka kupitia dirisha.

“Nilikuwa nimelala, nikahisi joto jingi, nikaamka. Moto mkubwa ulikuwa unawaka na kila mtu akawa anakimbia ndipo nilipoamua kurukia dirishani lakini nikiwa nje nilikumbuka rafiki yangu mwingine bado alikuwa ndani,’ alisema.

Baada ya kumuokoa mvulana wa kwanza aliyetoka akiwa na majeraha madogo ya moto mkononi, alimkumbuka mwingine aliyekuwa ndani amelala na bila kusita, tena kwa ujasiri licha ya hatari, akaingia tena ndani ya jengo hilo kumtoa mvulana mwingine wa Gredi ya Saba.

Hata hivyo, Karinga alisema hafahamu waliko wenzake hao wawili lakini Taifa Leo iligundua kuwa aliyechomeka mkono alitibiwa katika hospitali ya Mweiga Consolata na kuruhusiwa kuondoka.

Kwa kujitolea kwake, kukabiliana na hali ambazo zinaweza kuwashangaza watu waliofanya makubwa, amekuwa shujaa na familia yake inasema wanajivunia mtoto wao.

‘Nina furaha kwa mwanangu, ninamwona kama shujaa, alionyesha ushujaa na kufanikiwa kuokoa maisha ya wenzake,’ babake  Bw Ngumo alisema.

Bw Patrick Gikandi, mzazi katika shule hiyo anayetoka Kaunti ya Laikipia, pia alielezea vitendo vya kishujaa vya mwanawe Cleophas Kigochi.

Alisema mwanawe alikuwa miongoni mwa waliosaidia kuwaokoa wanafunzi wengine katika bweni lililokuwa likichomeka.

“Anasema aliamshwa na joto, na alipogundua wengi wa wanafunzi wenzake walikuwa wamelala, aliangusha sanduku lake, na akalitumia kuwatahadharisha wengi kadiri alivyoweza waelekee mahali salama. Wale waliokuwa karibu naye walitoka naye,” Bw Gikandi alisema kuhusu mwanawe Kigochi, mwanafunzi wa Gredi ya 8.

Wakati huo huo, jumla ya wanafunzi 70 wa shule hiyo walionusurika kwenye mkasa huo wa moto walitibiwa katika Hospitali ya Kaunti-ndogo ya Mt Kenya.

Kati ya waathiriwa, ni Karinga pekee aliyelazwa kwa uangalizi zaidi baada ya kubugiaa moshi kulingana na afisa mkuu wa hospitali hiyo Dkt Charles Ndirangu, akiongeza kuwa waliokuwa na majeraha madogo walifanyiwa ushauri wa kisaikolojia na kuunganishwa na wazazi wao.

Baadhi ya wakazi waliokuwa na ujasiri walilowesha mablanketi na kuingia motoni kuwaokoa wanafunzi wakati wa janga hilo.

Mnamo Jumamosi, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walifunga shule hiyo ambapo mkasa wa moto uliua wanafunzi 21 Alhamisi huku wanafunzi 10 wakilazwa katika hospitali mbalimbali katika Kaunti ya Nyeri wakipokea matibabu.

Maafisa hao, wakiongozwa na afisa wa kitengo cha kuchunguza mauaji, Bw Martin Nyuguto, walisema eneo hilo limefungwa, hata kwa wanahabari.

Kikosi hicho kinachojumuisha wataalamu wa maiti kilifanya mkutano Jumamosi asubuhi ili kupanga shughuli za uchunguzi pamoja na utoaji wa miili kutoka eneo la mkasa.