Wanafunzi katika shule 349 zilizozimwa kuwa na bweni lazima wahamishwe, wizara yasisitiza
WAZAZI walio na wanafunzi katika shule 349 ambazo zilizuiwa kuwa za bweni, wametakiwa kuwahamishia katika taasisi nyingine za masomo kabla ya shule kufunguliwa Jumanne wiki ijayo kutokana na masuala ya usalama.
Wizara ya Elimu iliwataka wazazi hao kuhakikisha watoto wao wanajiunga na shule tofauti baada ya ukaguzi uliofanywa kufuatia mkasa wa moto ulioua wanafunzi 21 kutoka shule ya Hillside Endarasha Academy miezi minne iliyopita kufichua masuala ya usalama katika shule hizo 349.
Ukaguzi ulibaini kuwa shule nyingi za msingi za bweni zinakabiliwa na changamoto za kiusalama na miundombinu ambazo zinahatarisha maisha ya wanafunzi.
Jumla ya shule 2,974 zilifanyiwa tathmini, ambapo 1,415 zilikuwa za umma na 1,659 za kibinafsi. Msongamano katika mabweni ulikuwa wa kawaida shuleni. Nafasi kati ya vitanda katika shule nyingi ilikuwa chini ya mita 1.2 kinyume na Mwongozo wa Viwango vya Usalama kwa Shule nchini Kenya (2008).
Shule chache hazikuwa na walinzi/ walezi wa mabweni ya wavulana. Katika baadhi ya shule, matroni walipewa majukumu katika mabweni ya wanafunzi wa kiume.
Katibu wa Elimu ya Msingi Belio Kipsang alisema serikali haitalegeza msimamo kuhusu agizo la kupiga marufuku baadhi ya shule kuwa za bweni. Alisema wazazi wa shule ambazo hazikidhi viwango vya usalama lazima wawahamishe wanafunzi hao.
“Tuliambia taasisi ambazo hazikuwa zimejitayarisha vya kutosha kuwa na bweni kuacha hadi wakati huo zitakapojitayarishwa ipasavyo. Na kila shule hizo 349 ilipewa ripoti ya kueleza ilichohitaji kufanya,” alisema Dkt Kipsang.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Dkt Kipsang alisema maafisa wa Wizara ya Elimu wamekagua tena baadhi ya shule.
“Shule yoyote ambayo imekidhi kiwango cha maandalizi itaruhusiwa kuendelea, lakini zile ambazo haziko tayari, tumewaambia wazazi watafute shule mbadala kwa watoto wao na tumewapa muda wa kutosha, karibu miezi miwili,” alisema.
Dkt Kipsang alisema maafisa wa wizara kwa sasa wanajumuisha data kuhusu ni shule ngapi za bweni ambazo bado hazijatimiza viwango vya usalama.
“Tuna mkutano wa wakurugenzi wetu wote wa kaunti ndogo, kaunti na maeneo leo, tutaweza kujua hali yoyote inayohitaji umakini maalum,” alisema.
Haya yanajiri huku wazazi wakiendelea kulalamika kuhusu hatua hiyo wakisema itakuwa changamoto na gharama kubwa kununua sare mpya, na huduma nyinginezo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa ya Wazazi Silas Obuhatsa alilaumu wazazi kwa kukosa kulazimisha bodi za usimamizi kuzingatia viwango vya usalama kabla ya shule kufunguliwa tena.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA