Wanafunzi wa Mawego walalamikia ukosefu wa usalama baada ya kuchoma kituo cha polisi
Mara tu baada ya kifo cha mwanablogu Albert Ojwang mnamo Juni 9, baadhi ya watu walikusanyika na kulenga maafisa wa usalama katika Kituo cha Polisi cha Mawego, Rachuonyo Kaskazini, Kaunti ya Homa Bay.
Lengo lao lilikuwa kuhakikisha maafisa wote wa kituo hicho wanahamishwa.
Siku moja kabla ya mazishi ya Ojwang mnamo Julai 3, baadhi ya vijana wakiwa na wanafunzi kutoka Chuo cha Ufundi cha Kitaifa cha Mawego, hatimaye walifanikiwa kufika katika kituo cha polisi.
Waliandamana kutoka Lida hadi kituoni wakiwa wamebeba jeneza la marehemu na kisha wakakiteketeza moto kituo hicho.
Jengo la mbao lililotumika kama ofisi ya kupokea ripoti na ofisi ya OCS liliungua hadi kuwa majivu.
Maafisa wengine wa polisi walipoteza mali yao baada ya umati kuvamia kituo hicho na kufanikiwa kuwafurusha maafisa waliokuwa humo.
Maafisa wote waliokuwa wakihudumu kituoni humo walihamishwa hadi Kituo cha Polisi cha Kendu Bay, umbali wa kilomita 16 kutoka hapo.
Kwa sasa, eneo hilo halina maafisa wa usalama wa kushughulikia dharura kutoka kwa wakazi, na inachukua takriban dakika 20 kusafiri kati ya maeneo hayo mawili mtu anapotaka kuripoti tukio.
Hali hii inawatia hofu wanafunzi wa chuo hicho cha ufundi ambao wamelalamikia kuongezeka kwa visa vya ukosefu wa usalama tangu kituo hicho kilipofungwa wiki tatu zilizopita.
Wanafunzi hao wameandika barua kwa Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Bw Raymond Omollo, wakimtaka atume maafisa kuhudumu katika kituo hicho na kuimarisha usalama.
Katika barua hiyo, rais wa chama cha wanafunzi Ephraim Were alidai kuwa wanafunzi kadhaa wamepoteza mali yao kwa wahalifu wanaotumia fursa ya kukosekana kwa polisi kuwapora.
‘Tumekumbwa na msururu wa visa vya uhalifu katika eneo hili. Tunajiandaa kwa mitihani na wanafunzi hawawezi kubaki shuleni kwa muda mrefu kwa masomo ya ziada wakihofia kushambuliwa,’ alisema.
Katika barua hiyo, kiongozi huyo wa wanafunzi alidai kuwa wahalifu walijaribu kumbaka mwanamke mzee katika eneo hilo.
Bw Were alisema kundi hilo halijafahamika.
Alisema wanafunzi wa chuo hicho ndio wanaoathirika zaidi kutokana na kutokuwepo kwa maafisa wa usalama.
‘Wanafunzi wa Mawego National Polytechnic wamekuwa wakikumbwa na visa vingi vya unyanyasaji kwa siku kadhaa, wengine huporwa simu na mali nyingine muhimu na watu wasiojulikana wanaotumia fursa ya kutokuwepo kwa polisi,’ aliandika Bw Were.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa wanafunzi, kuwepo kwa kituo cha polisi katika eneo hilo kutasaidia kukabiliana na visa vya uhalifu.
‘Tunaomba kwa unyenyekevu kituo cha polisi kirejeshwe kwa sababu tunaamini hatua hiyo itadhibiti ukosefu wa usalama katika eneo hili. Wanafunzi hulindwa tu na walinzi wa chuo wakiwa ndani ya taasisi. Mara tu wanapotoka nje, huwa wako hatarini,’ alisema Bw Were.
Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kaskazini, Bw Stephen Tanui, alisema hakuna yeyote aliyeripoti visa hivyo katika Kituo cha Polisi cha Kendu Bay.
Chuo cha Ufundi cha Kitaifa cha Mawego kina zaidi ya wanafunzi elfu saba, wengi wao wakiishi nje ya chuo.