Habari za Kitaifa

Wanafunzi wapata alama za juu KJSEA katika somo la Kiswahili

Na BENSON MATHEKA December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WANAFUNZI waliofanya Mtihani wa KJSEA wameng’aa katika somo la Kiswahili, ambalo limeibuka miongoni mwa masomo yaliyorekodi alama za juu zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Elimu wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani huo wa kwanza, zaidi ya asilimia 93 ya watahiniwa walizidi matarajio katika somo hilo, ishara ya kuimarika kwa umilisi wa lugha ya taifa.

Wataalamu wanasema utendaji mzuri katika Kiswahili unaakisi juhudi za walimu na wanafunzi katika kutekeleza mtaala unaolenga umilisi wa mawasiliano na matumizi ya lugha katika mazingira halisi.

Somo hilo pia lilikuwa miongoni mwa masomo ambayo wasichana waliwazidi wavulana kwa kiwango kikubwa, ambapo asilimia 64 ya wasichana walitimiza au kuzidi matarajio ikilinganishwa na asilimia 51 ya wavulana.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema matokeo haya yanaonyesha mafanikio ya utekelezaji wa mfumo wa CBE unaoweka uzito katika umilisi na vitendo.