Wanajeshi wa Jubbaland wamekita kambi Mandera, uchunguzi wa ‘Taifa Leo’ umebaini
LICHA ya Wizara ya Usalama wa Ndani kukana madai ya uwepo wa wanajeshi wa Jubbaland katika Kaunti ya Mandera, uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa wanajeshi hao wa kigeni wamekita kambi ndani ya ardhi ya Kenya.
Mwandishi wetu alizuru kata ya Border Point 1 (BB1), karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, na kushuhudia dalili za wazi kuwa wanajeshi hao wa Jubbaland wapo nchini kinyume cha sheria.
Bw Jibril Hussein Farah, mkazi wa eneo hilo, alitueleza kuwa wanajeshi hao wapo na tulipokuwa tukiondoka boma lake tulimwona mwanamume akiwa amevalia magwanda ya kijeshi akitembea kutoka upande wa Somalia.
Katika Shule ya Msingi ya Border Point 1 na Shule ya Sekondari ya Msingi ni wanafunzi wachache wamerejelea masomo ilhali shule zilifunguliwa rasmi Agosti 28 kwa masomo ya muhula wa tatu.
Duru katika shule hiyo iliambia Taifa Leo kwamba wazazi wengi wamechelea kuwaruhusu watoto wao kurejelea masomoni wakihofia athari za vita.