Wanakijiji waandamana kulalamikia kupuuzwa na wasimamizi wa uwanja wa ndege
Wakazi wa Olooloitikoshi, Kaunti ya Kajiado, Jumanne waliandamana dhidi ya usimamizi wa uwanja wa ndege wa kibinafsi wa Orly Airpark wakilalamikia ubaguzi wa rangi, ukosefu wa ajira, kucheleweshwa kwa miradi ya kijamii (CSR) na upanuzi wa njia ya kurukia ndege kwa miaka 25.
Mamia ya waandamanaji waliokuwa na mabango walitembea kutoka barabara ya Isinya-Kiserian hadi lango kuu la uwanja huo kushinikiza utekelezaji wa ahadi zilizotolewa tangu uwanja huo uanzishwe.
Wanasema kuwa licha ya kuvumilia kelele na hatari zinazotokana na ndege, jamii haijafaidika hata kidogo na uwepo wa uwanja huo.
Wenyeji pia wamelalamikia kuzuiwa kwa Kenya School of Flying kupanua eneo muhimu, hatua wanayosema imezuia ajira kwa vijana wa eneo hilo na kuhatarisha usalama wa marubani wanaojifunza.
Bi Nancy Kisoso, mmoja wa wakazi, alisema jamii ilikuwa na matumaini makubwa ya kunufaika na shule ya urubani lakini sasa mambo yamebadilika.
“Kupiga marufuku upanuzi wa barabara ya kurukia ndege kumezuia shughuli za shule ya urubani na kudhoofisha maisha ya vijana wetu ambao walikuwa wanapata mafunzo hapo,” alisema Bi Nancy Kisoso, mmoja wa wakazi.
Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Isinya, Bw Michael Yator, aliingilia kati na kuahidi kuitisha mkutano wa dharura kati ya serikali na wasimamizi wa Orly kushughulikia malalamishi hayo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Orly Airpark, Bw Christian Strebel, alisema kutotekelezwa kwa miradi ya CSR ni kwa sababu ya ukosefu wa fedha, akidai kuwa wawekezaji wanaodhibiti uwanja huo hawajalipa ada kwa miaka mingi.
Alikana madai ya ubaguzi wa rangi na upendeleo, akisema tayari wamemteua afisa wa mawasiliano wa jamii na kuwa upanuzi wa eneo la kupaa ndege ulikataliwa na wenyehisa kutokana na udongo hatari.
Wiki chache kabla ya maandamano, Captain Joseph Ririani – mwanzilishi wa Kenya School of Flying – alikosoa uamuzi wa kufunga sehemu ya njia ya kupaa ndege.
Orly Airpark ilianzishwa miaka ya 1990 kama kituo mbadala cha mafunzo baada ya msongamano katika Uwanja wa Wilson, lakini sasa imekumbwa na mivutano ya kijamii, kiusalama na kimaendeleo.
“Kwa miaka 25, hakuna mradi wowote wa maana wa kijamii uliotekelezwa hapa licha ya ahadi za mara kwa mara. Tumevumilia kelele za ndege, hatari, na sasa tunataka sauti yetu isikike,” ilisema sehemu ya malalamishi.