Habari za Kitaifa

Wanamazingira wataka kupanda miti kuwe ni mazoea, si kutenga tu siku moja moja

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

HUKU shughuli za upanzi wa miti zikiendelezwa sehemu mbalimbali nchini, wanamazingira wameifokea serikali kwa kuendeleza hulka mbaya ya uhifadhi nchini.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Ijumaa, wanamazingira hao wamesema wanataka kupanda miti kuwe ni mazoea na wala si kutenga tu siku moja moja kama inavyofanyika Kenya kwa sasa.

Wakiongozwa na Bi Rafa Aboud, wahifadhi hao walieleza kutamaushwa kwao na jinsi upanzi wa miti kwa minajili ya maadhimisho ya sikukuu fulani unavyoendeleza ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa washiriki wengi wa shughuli hizo.

“Utapata watu hawajitumi wenyewe binafsi kupanda miti na kutunza mazingira yao. Lakini punde siku maalumu inapotangazwa, hawa hawa watu ndio wanajitokeza kwa wingi kupanda miti Na kuweka picha mitandaoni kujisifu. Punde maadhimisho yanapofikia tamari,huo pia unakuwa mwisho wao wa uhifadhi. Hakuna ufuatilizi wa aina yoyote kujua Je,miche imemea na kukua vipi. Utapata miche mingi inaishia kunyauka na kufa bila uangalizi wa yeyote,” akasema Bi Aboud.

Bi Rafa Aboud, mhifadhi na mpenda mazingira kisiwani Pate, Lamu Mashariki. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Aboud ni miongoni mwa makundi machsche ya akina mama waliojitolea kuendeleza upanzi na uhifadhi wa mazingira kisiwani Pate,Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki tangia udogoni mwao.

Naye Bi Husna Bakari, alishikilia kuwa upanzi wa miti wafaa kuwa kwa hiari ya mtu na wala si kwa kulazimishwa.

Anasema punde mtu anapojituma mwenyewe bila kusubiri amri,iwe ni ya serikali,mashirika au maadhimisho ya siku maalumu, huwa anakuwa na ule moyo wa kufuatilia kuhakikisha juhudi zake zinazaa matunda.

Bi Bakari anatoa mfano wa jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni Lamu ambao tangu jadi ja jadi wamezaliwa na kukuzwa wakiona wazazi na mababu zao wakijituma katika kuhifadhi misitu,hasa mikoko.

“Tujizoeshe kupanda na kukuza miti na kuhifadhi mazingira yetu bila kusubiri hadi maadhimisho ya siku fulani au amri ya serikali ndipo tufanye hivyo. Tukilazimishwa kuwajibikia jukumu hili hatutafaulu,” akasema Bi Aboud.

Mwenyekiti wa Makundi ya Kijamii ya Kuhifadhi Mikoko na misitu (CFAs), kaunti ya Lamu, Bw Abdulrahman Aboud Lali, alisifu wanajamii Lamu kwa kuwa kielelezo cha kutunza na kuhifadhi mazingira kote nchini.

Bw Lali anasema wakazi wa Lamu wameifanya kuwa kawaida kwao kama ibada kupanda na kuhifadhi misitu,hasa ile ya mikoko eneo lao.

Kaunti ya Lamu inaongoza kwa kuwa na asilimia zaidi ya 60 ya misitu ya mikoko ipatikanayo kote nchini.

“Jamii yetu ya Wabajuni huwa haisubiri tangazo la serikali ndipo ijitume katika upanzi wa miti au uhifadhi wa mazingira. Sisi hutekeleza jukumu hilo karibu kila siku. Ikiwa site nchini na ulimwenguni tutaendeleza hulka hiyo,Kenya na Ulimwengu utakuwa sehemu nzuri ya binadamu na viumbe vingine kuishi na kumaliza kabisa hili tatizo linalotukimba la mabadiliko ya tabia nchi,” akasema Bw Lali.

Mnamo Ijumaa, upanzi wa miti umeendelea katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Murang’a, Trans Nzoia, Kirinyaga, Kajiado na Siaya miongoni mwa kaunti nyingine.

Rais William Ruto aongoza hafla ya kitaifa ya upanzi wa miti ambapo hapa anaonekana akipanda mche wa mti ndani ya msitu wa Kiambicho kwenye mlima unaofahamika kama Karua Hill A,  Kaunti ya Murang’a. PICHA | JOSEPH KANYI

Rais William Ruto ameongoza hafla ya kitaifa ya upanzi wa miti ambapo amepanda mti ndani ya msitu wa Kiambicho kwenye mlima unaofahamika kama Karua Hill A,  Kaunti ya Murang’a.

Naye Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amekuwa katika Kaunti ya Trans Nzoia kwa shughuli hiyo ya upanzi wa miche ya miti.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu akipanda miti katika msitu wa Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia. PICHA | OSBORN MANYENGO

Mei 10 ilichapishwa kwa Gazeti Rasmi la Serikali kuwa ni siku ya kuonyesha mshikamano na waliopoteza maisha yao kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.