Wanane wakamatwa, gari la msafara wa Ruto likiua raia jijini
POLISI wamewakamata watu wanane wanaoshukiwa kuhangaisha watu katika barabara ya Thika wakati wa ziara ya Rais William Ruto siku mbili zilizopita.
Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema kwamba walianzisha msako mkali ili kuwakamata na kulishtaki genge lililowashambulia na kuwaibia Wakenya wasio na hatia.
Kulingana na DCI, wanane hao ni miongoni mwa kundi la watu 10 walioibia umma simu zao na vitu vingine vya thamani katika eneo la Mathare Area 4.
“Kufikia sasa, John Junior Oginga, ambaye alikuwa amejihami kwa kisu alipomvamia na kumpora mtu simu ya mkononi aina ya Oppo A77S ya thamani ya Sh28, 000, alikamatwa. Oginga alikamatwa kwenye Barabara kuu ya Thika na kupelekwa hadi Kituo cha Polisi cha Pangani,” DCI ilisema kwenye taarifa.
Washukiwa wengine ni pamoja na Jared Nyanza, Darlin Lande, Daniel Okombe, Mike Robert, Elvis Otieno, Reagan Omondi na Mathenge Gachiri.
Washukiwa hao walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga na baadhi ya vitu ambavyo vilipatikana kutoka kwao ni pamoja na nguo mpya zinazoaminiwa kuwa mali ya wizi.
“Washukiwa wote walifikishwa mahakamani. Wakati huo huo, maafisa wa Polisi wameimarisha msako mkali ili kuwafikisha mahakamani washukiwa wengine waliobaki waliohusika na vitendo hivi vya uhalifu.”
Wakati wa ziara ya Rais katika eneo bunge la Mathare, waliokuwa wakitembea na madereva kadhaa walipoteza vitu vyao vya thamani huku genge hilo likisababisha uharibifu licha ya ulinzi mkali uliowekwa katika eneo hilo.
Tukio kama hilo pia liliripotiwa katika eneo la Kamukunji, ambapo watu walivamiwa mara tu baada ya Rais kumaliza hotuba yake.
Pia, tukio sawia liliripotiwa Jumatano katika eneo la Kawangware wakati wa ziara ya Rais, ambapo watu walipoteza vitu vyao vya thamani huku magenge hayo yakiwaibia Wakenya mchana.
Wakati uo huo, mtu mmoja aliaga dunia Alhamisi mwendo wa saa nne asubuhi, baada ya kugongwa na mojawapo wa magari yaliyokuwa kwenye msafara wa rais katika Barabara ya Ngong, Adams Arcade.
Ajali hiyo ilitokea msafara wa Rais Ruto ulipokuwa ukielekea maeneo bunge ya Lang’ata na Kibra.
Kulingana na polisi, ajali hiyo ilihusisha raia wa kigeni ambaye bado hajulikani ni nani.
“Kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea leo katika eneo la Adams Arcade kando ya Barabara ya Ngong iliyohusisha gari la serikali na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye ni raia wa kigeni, Jeshi la Polisi sasa linashughulikia suala hilo na uchunguzi umeanza,” ilisema taarifa hiyo.