Wanaokaidi wazee kufungwa jela mswada ukipitishwa bungeni
KUKAIDI uamuzi wa Baraza la Wazee kunaweza kukufanya ufungwe jela miezi sita na kutozwa faini ya Sh50,000 iwapo mswada unaojadiliwa kwa sasa Bungeni utapitishwa.
Mswada wa Baraza la Wazee, 2024, unaofadhiliwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, unalenga kuweka mfumo wa kisheria wa utatuzi mbadala wa migogoro ndani ya jamii, utakaosimamiwa na mabaraza ya wazee katika kila koo.
“Viongozi wa kimila wakiwemo wazee wa kiume na wa kike wana mchango mkubwa katika usimamizi wa migogoro inayohusiana na maliasili, utatuzi wa migogoro na baraza la wazee unatokana na taratibu zinazoeleweka na kukubalika na jamii ili watu waweze kutii maamuzi yao,” mswada huo unasema.
Mswada huo unaambatana na Kifungu cha 159 cha Katiba, ambacho kinatambua jukumu la kitamaduni la wazee katika kutatua mizozo ya kijamii.
Sheria inayopendekezwa inalenga matumizi ya utatuzi mbadala wa migogoro kama njia ya kusuluhisha mizozo ili kuondoa mrundiko wa kesi katika mahakama.
Bw Barasa anahoji kuwa ingawa Mswada hautapunguza mrundiko wa kesi katika mahakama, utakuwa na gharama nafuu na kutoa haki kwa Wakenya wengi wanaotatizika.
Baraza la Wazee linalopendekezwa litakuwa na mwenyekiti, naibu mwenyekiti, katibu, kiongozi mwanamke, kiongozi wa vijana na kiranja mkuu.
Baraza la Wazee litachaguliwa na jamii kwa muda wa miaka mitatu, unaoweza kufanywa upya mara moja.
Baraza la Wazee litakuwa na mamlaka ya kusuluhisha migogoro, kumwita mtu yeyote kutoa ushahidi kuhusiana na kesi inayofikishwa mbele yake na pia kutoa maagiza kuhusiana na kesi zinafikishwa mbele yake.
Mswada huo unapendekeza wazee hao walipwe marupurupu ya Sh24,000 kwa mwezi.
Mnamo Juni, Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Raymond Omollo aliambia kamati ya bunge kwamba itagharimu walipa ushuru Sh2.7 bilioni kila mwezi kuwalipa wazee wa vijiji ikiwa Mswada wa Marekebisho ya Serikali ya Kitaifa (Marekebisho) wa 2024 utapitishwa na Bunge.
Dkt Omollo aliteta kuwa ikiwa serikali itaajiri angalau wazee wa vijiji watano katika kila kaunti ndogo kwa malipo ya kila mwezi ya Sh5,000, itagharimu serikali Sh226 milioni kila mwezi, ambazo ni Sh2.7 bilioni kila mwaka.
Mswada huo unampa mamlaka Jaji Mkuu, polisi na machifu kupeleka kesi kwenye Baraza la Wazee huku jaji mkuu akitoa kanuni za kesi zinazopelekwa barazani.
Iwapo utapitishwa, mswada huo utaimarisha nafasi ya baraza la wazee katika jamii kama chombo muhimu kinachoongoza kuwakilisha koo na koo ndogo.
Katika maeneo ya vijijini, mabaraza ya wazee yana jukumu muhimu katika kuhakikisha uwiano wa kijamii ndani ya jamii, kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kutatua mizozo tata.
Kwa mfano, mnamo 2016, wazee 60 kutoka Kaunti ya Nyeri walitumiwa kusaidia idara ya mahakama katika kutatua kesi ndogo ndogo, nyingi zilizohusisha mizozo ya kifamilia na ardh