Wanawake 129 wauawa tangu Januari, Kaunti hatari zaidi zatambuliwa
TAKRIBAN wanawake 129 wameuawa kote nchini kati ya Januari na Machi mwaka huu, huku visa vingi vya mauaji katika kaunti za Busia, Pokot Magharibi, na Nandi vikihusisha waathiriwa wanawake pekee.
Mwezi wa Machi ulirekodi idadi kubwa zaidi ya vifo vya wanawake kwa visa 44, ukifuatwa na Januari (43) na Februari (42). Kulingana na takwimu za 2024, wanawake 579 waliripotiwa kuuawa ikilinganishwa na 534 mwaka uliopita na 526 mwaka 2022.
Ripoti za Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC), zilizowasilishwa wakati wa kikao cha Jopo Kazi la Kiufundi kuhusu Ukatili wa Kijinsia (GBV) na Mauaji ya Wanawake, zinaonyesha kuwa wanaume ndio waliohusika na asilimia 85 ya visa hivyo. Wanawake walihusika na asilimia 10, huku asilimia 5 wakiwa wauaji wasiojulikana.
Visa vya wanawake kuua viliongezeka Nairobi (21) na maeneo ya Kati (19). Kaunti za Kisumu, Kilifi, na Nairobi ziliripoti mauaji mengi ya wanawake ambapo wauaji hawakujulikana.
Mkurugenzi wa masuala ya Jamii, Jinsia na Ulinzi wa Watoto katika NPS, Judy Lamet, alisisitiza haja ya kuanzishwa na kupanuliwa kwa vitengo vya kushughulikia ukatili wa kijinsia katika vituo vyote vya polisi. Pia alitoa wito kwa mafunzo maalum kwa maafisa wa polisi kuhusu jinsi ya kushughulikia waathiriwa wa unyanyasaji kwa njia ya kihisia na usimamizi bora wa maeneo ya uhalifu.
NPS ilipendekeza fomu za P3 na huduma za baada ya ubakaji ziwe dijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma na ukusanyaji wa ushahidi. Aidha, maafisa wa polisi wapelekwe katika hospitali za kiwango cha nne ili kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu kwa waathiriwa.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa NPS, Amos Omuga, alipendekeza kuanzishwa kwa mahakama maalum za kushughulikia kesi za GBV na mauaji ya wanawake katika kila kaunti. Alisisitiza pia haja ya kufanya dijitali njia za kuripoti GBV ili waathiriwa waweze kuwasiliana na Idara za usalama haraka na kwa siri.
“Sheria zipo, lakini utekelezaji wake una matatizo makubwa. Vitengo kama Kitengo cha Masuala ya Ndani na IPOA vinapaswa kuchunguza maafisa wote wanaoshindwa kushughulikia kesi hizi kwa weledi,” alisema Omuga.
Mkurugenzi wa NCRC, Dkt Mutuma Ruteere, alisema kuwa Bonde la Ufa linaongoza kwa visa vya mauaji ya wanawake kwa visa 66, ikifuatiwa na Mashariki (51) na Magharibi (42). Kaskazini Mashariki ilikuwa na idadi ndogo zaidi – visa nane pekee.
Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa vya mauaji ya wanawake kwa visa 19, ikifuatiwa na Kiambu (17), Kilifi (16), na Trans Nzoia (13). Katika kaunti za West Pokot na Nandi, waathiriwa wote wa mauaji walikuwa wanawake. Busia ilikuwa na visa nane vya mauaji, saba kati ya waathiriwa wakiwa wanawake.
Dkt.Ruteere alifichua kuwa asilimia 50 ya mauaji ya wanawake yalitokana na migogoro ya kifamilia, asilimia 30 sababu hazikujulikana, asilimia 5-10 zilihusishwa na tuhuma za uchawi, na asilimia 5 zilihusiana na mizozo ya ardhi.