• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wanawake wanaongoza kukopa pesa jamaa na marafiki maisha yakilemea wengi – Utafiti

Wanawake wanaongoza kukopa pesa jamaa na marafiki maisha yakilemea wengi – Utafiti

NA WANDERI KAMAU

WAKENYA sasa wamegeukia kuwakopa jamaa na marafiki wao kutokana na ugumu wa hali ya maisha, huku wanawake wakiongoza kwa mtindo huo.

Kulingana na utafiti uliotolewa Jumatatu na shirika la Infotrak Harris, asilimia 52 ya wanawake walisema wamegeukia ukopaji fedha kutoka jamaa na marafiki, ikilinganishwa na asilimia 44, ambao ni wanaume. Kijumla, ni asilimia 48 ya Wakenya ambao wamegeukia ukopaji.

Shirika lilisema mtindo huo ni baadhi ya mbinu kadhaa ambazo Wakenya wamevumbua, ili kukabiliana na ugumu wa hali ya kimaisha.

Asilimia 24 walisema wamekuwa wakisaidika kutokana na mipango inayoendeshwa na serikali, asilimia 19 kutoka kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), asilimia 12 walisema wamekuwa wakipata usaidizi wa kifedha kutoka kwa shughuli tofauti kwenye mitandao, asilimia kumi kwenye mikakati inayoendeshwa na waajiri wao kuwasaidia wafanyakazi, asilimia nane wakasema hawana usaidizi wowote huku asilimia moja wakilazimia kuuza mali yao.

Utafiti huo ulieleza kuwa asilimia 73 ya Wakenya wanakabiliwa na matatizo ya kifedha, wakisema imekuwa vigumu kwao kutimiza mahitaji yao ya kimsingi kama vile kupata chakula, mavazi au kodi ya nyumba.

Kati ya Wakenya hao asilimia 73–asilimia 18 kati yao wanakabiliwa na hali ngumu zaidi kifedha, huku asilimia 55 wakikumbwa na changamoto kutimiza mahitaji ya msingi.

Ni asilimia tano pekee waliosema wanaishi katika hali nzuri bila kuhangaika kifedha, huku asilimia 22 wakieleza kutoona mabadiliko yoyote maishani mwao.

Kutokana na hali hiyo, asilimia 45 walisema  wamelazimika kufanya kazi mbadala ili kuboresha mapato yao, huku asilimia 41 wakilazimika kupunguza matumizi yao katika masuala yasiyo muhimu.

Utafiti huo ulisema asilimia 18 ya Wakenya wamelazimika kuchukua mikopo ili kushughulikia matatizo ya kiuchumi yanayowakabili.

Hayo yakijiri wakati serikali inasisitiza inafanya kila iwezalo kuboresha hali ya uchumi nchini, Wakenya wengi walisema hali hizo zimewaletea athari za kiafya.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 48 ya Wakenya walisema wanakumbwa na wasiwasi na masumbuko ya kimawazo, asilimia 32 wakasema hali hizo zimeathiri mahusiano na wapenzi au marafiki wao wa karibu, asilimia 21 wakaeleza wameathirika kiafya mwilini huku asilimia 18 wakikumbwa na matatizo ya afya ya kiakili.

  • Tags

You can share this post!

Ruto sasa aahidi kutii maamuzi ya mahakama

Mwanamume asimulia jinsi kuoa mapema kumemzimia nyota ya...

T L