Wandani wa Lissu wanyakwa wakienda kortini kusikiza kesi
DAR ES SALAAM, TANZANIA
POLISI jana waliwazuilia wanasiasa wawili wakuu wa CHADEMA ambao walikuwa wakielekea kortini wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu.
Wawili hao walikuwa wakiendesha magari yao binafsi walipobambwa huku Lissu akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Uongozi wa CHADEMA ulithibitisha kukamatwa kwa katibu wake John Mnyika na Naibu Mwenyekiti John Heche.
Kwa mujibu wa Msemaji wa chama Brenda Rupia, wawili hao walikuwa wakielekea katika Mahakama ya Hakimu ya Kisutu. Bw Rupia alilalamika kuwa haki zao zilikiukwa.
“Tunaendelea kushuhudia ukiukaji wa haki za kibinadamu, uhuru wa kujieleza na kuvunjwa kwa sheria. Hatutaruhusu nchi yetu irejeshwe kwenye enzi za utawala giza ambao dhuluma, vitisho na viongozi waliuziwa uoga,” akasema Rupia.
Sababu ya kuzuiliwa kwa wawili hao haikufahamika na polisi hawakuwa wametoa taarifa zao kuhusu suala hilo. Lissu ambaye aliibuka wa pili kwenye uchaguzi wa 2020 alishtakiwa kwa uhaini mwezi uliopita.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa alitoa hotuba ya uchochezi akiwataka raia wa Tanzania wasusie na wavuruge uchaguzi wa urais na ubunge ambao unatarajiwa kuandaliwa mnamo Oktoba, 2025.
Kortini, hakuruhusiwa kujibu mashtaka ya uhaini lakini alikanusha shtaka jingine la kuchapisha habari za uongo. Siku chache baada ya kushtakiwa kwake, Tume ya Uchaguzi nayo ilipiga marufuku Chadema kushiriki kura hiyo.
Tume hiyo ilidai Chadema haikutia saini stakabadhi ya mwongozo wa kura hiyo kwa wakati. Ingawa hivyo, Chadema ilikanusha hilo japo ilikuwa imetishia kususia kura hiyo iwapo sheria za uchaguzi zisingefanyiwa marekebisho.
Chama hicho kinadai kwamba sheria za sasa zinapendelea CCM. Lissu alinusurika kifo baada ya kupigwa risasi mara 16, na siasa zake zimeanika utawala Rais Suluhu kama ule usio wa kidemokrasia na usiozingatia haki.