Habari za Kitaifa

Washirika wa Gachagua mbioni kuunda chama watakachotumia kumtoa jasho Ruto

November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameunda vyama vipya vya kisiasa huku kukiwa na fununu kuhusu uwezekano wake kuungana na viongozi wa upinzani unaoongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Taifa Leo imefahamu kuhusu msururu wa mikutano ya faragha iliyohusisha Bw Gachagua, Bw Musyoka na kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa kupanga mikakati dhidi ya Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Viongozi hao watatu wanasemekana kukutana angalau mara mbili baada ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua, kulingana na washirika wao.

Katika mikutano hiyo, viongozi hao wanasemekana kuwazia kutema Azimio La Umoja One Kenya ili kuunda muungano mpya watakaoutumia katika uchaguzi ujao. Pia kulikuwa na pendekezo la Azimio kubadilishwa ili kushughulikia masilahi ya wanachama wapya.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, ambaye amekuwa mmoja wa watetezi wakali wa Bw Gachagua, alithibitisha kwamba ana chama cha kisiasa. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) imekubali usajili wa muda kwa angalau vyama saba vipya vya kisiasa.

Bw Waititu, hata hivyo, alifafanua kuwa Bw Gachagua hana uhusiano na chama chake. Pia alikataa kutaja chama hicho.

Gavana huyo wa zamani ambaye aliondolewa madarakani na kuzimwa kugombea wadhifa katika uchaguzi ujao, alifichua kwamba hivi karibuni atazindua chama chake.

“Tayari nina chama cha kisiasa kilichosajiliwa,” alisema. Pia alithibitisha mazungumzo ya muungano kati ya Bw Gachagua na Bw Musyoka.

Katika mahojiano tofauti, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo kwamba, Bw Waititu ametwaa chama cha Kenya Reform Party (KRP), ambacho ni mshirika wa Azimio La Umoja One Kenya Coalition.

Msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alisema afisi yake bado haijapokea mawasiliano yoyote kuhusu mabadiliko yoyote ya uongozi katika chama hicho.

“Pengine wawe na mazungumzo hayo huko nje, hatujapata maombi rasmi ya mabadiliko yoyote ya uongozi,” alisema Bi Nderitu. Rekodi za ORPP zinaonyesha kuwa kuna vyama saba vya siasa ambavyo vimepata usajili wa muda.

Hivi ni pamoja na Kenya Ahadi Party (KAP) kilichosajiliwa Oktoba 16, 2024, Imarisha Uchumi Party (IUP), kilichosajiliwa Juni 24, 2024 na Peoples Forum for Rebuilding Democracy (PFRD), kilichosajiliwa Juni 13, 2024.

Vingine vilivyosajiliwa kwa muda ni National Economic Development Party (NEDP), The We Alliance Party (TWAP) na Kenya Liberals Alliance (KLAP).

Bw Gachagua Jumatatu alivuliwa rasmi wadhifa wa naibu kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), na nafasi yake ikachukuliwa na Naibu Rais Kithure Kindiki.