Habari za Kitaifa

Washukiwa wa mauaji ya Rita Waeni, raia wa Nigeria walinunua shoka mtandaoni – Polisi

January 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JOSEPH NDUNDA

RAIA wawili wa Nigeria wanaoshukiwa kumuua na kumkatakata kwa vipande msichana wa chuo kikuu karibu na TRM, Kasarani, na kutoweka na kichwa chake, wamo nchini kinyume na sheria, upelelezi wa DCI umebaini.

William Ovie Opia paspoti yake ilishakwisha muda na Johnbull Asbor ambaye DCI wanasema hakuwa na stakabadhi zozote za usafiri wakati alipokamatwa. Asbor aliambia polisi kwamba alipoteza paspoti yake miaka miwili iliyopita.

Washukiwa hao walinaswa kwenye nyumba moja eneo la Ndenderu, Kiambu, Jumapili.

Kachero Benjamin Wangila kutoka DCI Kasarani aliambia Mahakama ya Makadara kwamba wawili hao walikuwa wanaishi karibu na eneo ambalo kichwa kinachoshukiwa kuwa cha Rita Waeni kilipatikana.

Soma Maafisa wasaka kichwa cha Rita Waeni

Halafu Familia yaeleza jinsi binti yao wa miaka 20 aliuawa kikatili Roysambu

Shoka, kisu kikubwa, kitambulisho cha kitaifa cha Mkenya mmoja, simu sita, kipakatalishi, sim kadi 10 za mashirika mbali mbali ya simu na bidhaa zingine zilinaswa kwenye nyumba walimokutwa washukiwa hao.

“Kikosi cha upelelezi kinatafuta rekodi za simu zote zilizopigwa kutumia sim kadi na nambari za simu zilizokutwa kwenye simu kubaini iwapo walihusika na mauaji hayo,” alisema Wangila kwenye ushahidi kortini.

“Tunahitaji muda wa kutosha kupeleka washukiwa katika maabara ya serikali kupata sampuli za damu kwa ajili ya vipimo vya DNA ili kulinganisha na sampuli zilizokusanywa kwenye eneo la mkasa.”

Alisema washukiwa wanaweza kutoroka wakiachiliwa kwa sababu hawana makazi maalum kwa kuwa ni wageni nchini.

Wangila alikuwa anaomba mahakama iwape muda wa kuzuilia washukiwa kwa siku nane zaidi katika kituo cha polisi cha Kasarani, na wakakubaliwa kufanya hivyo na Hakimu Mkuu Agnes Mwangi wa Mahakama ya Makadara.

Wawili hao sasa watazuiliwa hadi Januari 31.

Rekodi za kortini zinaonyesha kwamba Opia alinunua shoka kutoka kwa duka la mtandaoni na kwamba aliambia polisi lilikuwa la kujilinda.

Wangila anasema wanachunguza pia kosa la mauaji dhidi ya mmiliki wa nyumba hiyo ya kuishi kwa muda eneo la Roysambu, ambako Rita aliuawa.

Bi Maina ambaye amekuwa kizuizini tangu kuripotiwa kwa tukio hilo Januari 14 aliambia polisi kwamba alipokea habari kutoka kwa mlinzi wa nyumba hiyo kwamba kulikuwa na michirizi ya damu kutoka kwa nyumba iliyoelekea hadi eneo la kutupa taka ambapo sehemu za mwili zilipatikana zimefungwa na karatasi. Kichwa hakikuwepo.

Bi Maina anazuiliwa kwa kukosa kuanakili habari muhimu za wapangaji wake, kama inavyohitajika kisheria na haswa jinsi zingesaidia kunasa washukiwa.

Familia ya Waeni ilishindwa kutambua kichwa kilichopatika na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City.

Rekodi katika mochari hiyo zinaonyesha kwamba kichwa hicho ni cha mwanamke ingawa haijatambuliwa ni nani.

Simu pia iliyopotea ya mwathiriwa ilipatikana kwenye eneo hilo. Kichwa hicho kilipatikana kimefungwa kwa gunia na kuzungushiwa blauzi ya rangi ya zambarau, jambo linaloibua maswali zaidi kuhusu tukio hilo la kusikitisha.

Upasuaji uliofanyiwa mwili huo Ijumaa iliyopita ulionyesha kwamba kucha zake pia hazikuwepo.